December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zambia kushirikiana na hospitali ya rufaa ya kanda ya Mbeya utoaji huduma za afya

Na Mwandishi wetu, Timesmajira, Online, Zambia

HOSPITALI ya Taifa ya Zambia imeonesha nia ya kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya katika utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi Zambia kwa lengo la kubadilishana uzoefu na ujuzi wa utoaji huduma bora wa huduma za afya.

Akizungumza baada Uongozi wa hospitali ya rufaa ya Kanda ya Mbeya kutembelea hospitali ya Taifa ya Zambia pamoja na Uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Zambia Dkt. Lazaro Mboma mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa MZRH leo amesema lengo la ziara hiyo ni kushirikiana utaalamu katika utoaji wa matibabu bora na sahihi kwa wananchi na ukuzaji wa teknolojia ya tehama katika kuimarisha upatikanaji wa kumbukumbu sahihi.

Aidha Dkt.Mboma amesema matibabu kwa mfumo wa e-Medical ikiwa ni pamoja na tiba mtandao ili kurahisisha utendaji kazi na kuongeza ufanisi kukiwemo kukuza uhusiano wa muda mrefu kati ya watoa huduma za afya

“Tunapenda kuushukuru uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Lusaka Zambia kwa kutupokea na kutupa fursa ya kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali za matibabu na huduma bora za afya. Tunaamini kuwa ziara hii itasaidia kuboresha huduma za afya katika zetu na kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya afya nchini zetu”amesema Dkt. Mboma.

Dkt. Mboma ameeleza kuwa ushirikiano huo unajumuisha kutoa huduma za matibabu kwa wagonjwa kutoka nchi zote mbili wanaohitaji matibabu maalum ambayo hayapatikani katika hospitali zao za ndani, vilevile kubadilishana wataalamu wa afya kati ya hospitali zote mbili kupitia programu za mafunzo mtambuka ya kubadilishana wataalamu.

Nae Dkt. Musaku Mwenechanya Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Taifa ya watoto Zambia ameeleza kuwa hospitali hiyo inatarajia kuwa ushirikiano huo utaleta manufaa makubwa kwa hospitali zote mbili na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi wa nchi hizi mbili na wako tayari kuwapokea wataalamu wetu na kuendela kushirikiana kwa karibu katika siku zijazo.

“Tunafuraha ya kuanzisha ushirikiano huu na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya mpango huu utatuwezesha kutumia nguvu na rasilimali za kila taasisi ili kunufaisha jamii tunazohudumia.” -Dkt. Musaku

Nae Balozi wa Tanzania Nchini Zambia Mhe. Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule amepongeza hatua zilizofikiwa kwa hospitali zote mbili katika ufanikisha ushirikiano huu kuwa Mataifa yote mawili yamekuwa na uhusiano mkubwa baina ya nchi kwa miaka mingi sasa kupitia waasisi wake, na anaimani kuwa ushirikiano huu utaimarisha zaidi uhusiano huo na kutazamia kubadilishana mbinu bora katika utoaji na usimamizi wa huduma za afya.

Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya kutangaza tiba utalii(Medical Toursim) kitaifa na kimataifa, na inatoa huduma za kibingwa na vipimo mbalimbali zikiwemo huduma za upasuaji wa kibingwa kama vile upasuaji wa moyo, ubongo na uti wa mgongo, figo, ini,.

Amesema pia upasuaji wa mdogo na matibabu ya saratani, huduma za magonjwa ya akili na matibabu ya kisaikolojia, huduma za magonjwa ya wanawake kama vile matibabu ya uzazi na matibabu ya magonjwa ya kizazi, huduma za upasuaji wa mifupa na mishipa ya damu, huduma za magonjwa ya kisukari na magonjwa ya figo.