January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zahanati yakamilika baada ya miaka tisa

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa Zahanati ya kijiji cha Fyengeleza iliyoanzishwa kujengwa kwa nguvu za wananchi mwaka 2013

Sababu iliyochelewesha ukamilishaji wa ujenzi huo ni Changamoto ya upatikanaji wa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.

Akizungumza leo wakati alipotembelea kuona mradi huo ulioanza kazi ya kutoa huduma za afya ,Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti ameupongeza uongozi wa halmashauri hiyo kwa kutoa fedha kukamilisha mradi huo.

“Mkurugenzi na timu yako nawapa pongezi kwa kukamilisha mradi huu muhimu kwa ustawi wa wananchi. Sasa huduma zinapatikana hapa karibu na makazi yao” alisema Mkirikiti

Katika hatua nyingine Mkirikiti aliagiza Wakala wa Maji Vijijini ( Ruwasa) kukamilisha miundombinu ya maji kwenye zahanati hiyo mapema ili kuwezesha huduma kuwa bora.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa ameuagiza uongozi wa kata na kijiji cha Fyengeleza kupanda miti kwenye eneo hilo ili kuhifadhi mazingira na kuanzisha mradi wa benki tofali ili kuwezesha ujenzi wa nyumba za waganga kituoni hapo.

” Diwani nataka kuona ukihamasisha wananchi wapande miti kwenye eneo hili la zahanati ili kutunza mazingira na kuhifadhi uoto wa asili” alisema Mkirikiti

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisema halmashauri imejipanga kukamilisha kazi zilizosalia ambapo fedha zipo na mafundi wanaendelea na kazi hiyo

.Mtalitinya alitaja gharama mradi huo kuwa ni shilingi Milioni 125 ambapo kati yake nguvu za wananchi ni shilingi Milioni 25, halmashauri ilitoa shilingi Milioni 40 na serikali kuu shilingi Milioni 60 .

Akitoa shukrani kwa kwa niaba ya wananchi mkazi wa Fyengeleza Jackilina Masanja alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kukamilisha mradi huo ambao tayari huduma zimeanza kutolewa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti yuko katika ziara kukagua na kuhamasisha shughuli za maendeleo ambapo awali amekagua mradi wa maji wa kijiji cha Mponda ambao umegharimu shilingi Milioni 280.