March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yazindua huduma ya macho bure Sabasaba

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas, imezindua rasmi huduma ya bure ya macho kwa wananchi wote wanaotembelea banda lake katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam.

Huduma hiyo, inatolewa kwa kushirikiana na KSI Charitable Eye Centre, ikijumuisha Uchunguzi wa macho.

Zingine ni, Upimaji na ugawaji wa miwani bure, Matibabu ya matatizo kama mzio, vumbi na Rufaa kwa wagonjwa wenye mtoto wa jicho wanaohitaji upasuaji.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Mahusiano ya Nje wa Yas, Rukia Mtingwa alisema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo ya kuwa mshirika wa kweli wa maendeleo ya jamii ya Kitanzania.

“Kuona ni haki ya msingi ya kila binadamu. Kwa bahati mbaya, Watanzania wengi hususan wa kipato cha chini na wanaoishi vijijini au kwenye maeneo yenye huduma hafifu za afya, wanakosa huduma za macho.

“Yas tumeamua kuja kivingine si tu kama mtoa huduma za mawasiliano, bali kama mshirika wa maisha ya kila siku ya Mtanzania,” alisema Mtingwa.

Huduma hiyo ni sehemu ya kampeni ya “Afya ya Macho kwa Wote”, iliyoanzishwa na Yas mwaka jana.

Tangu kuanzishwa kwake, kampeni hiyo imewafikia zaidi ya wananchi 25,000 katika mikoa ya Tanga, Mbeya, Mtwara, Pwani, Unguja na Pemba. Yas inatarajia kuwafikia maelfu zaidi kupitia maonesho ya mwaka huu.

“Kama kampuni ya kidijitali, tunaamini hakuna maana ya teknolojia kama mtu hawezi kuona. Teknolojia bila afya ni sawa na mwanga bila macho. Ndio maana tumechukua hatua za makusudi kusaidia jamii kwa vitendo,” alisisitiza.

Huduma ya macho itatolewa kila siku katika banda la Yas hadi kufikia mwisho wa maonesho ya Sabasaba, ikiwa wazi kwa wananchi wote bila gharama yoyote.

Mtingwa pia, alitoa shukrani kwa KSI Charitable Eye Centre kwa utaalamu wao wa hali ya juu na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya na TAMISEMI kwa kuruhusu huduma hii kufanyika kwa mafanikio makubwa.

“Uoni bora si afya tu ni fursa ya kuona familia yako, kujifunza, kufanya kazi, kuendesha biashara, na kutumia huduma za kidijitali kama Yas na Mixx. Tunawakaribisha wote kwenye banda letu,” alihitimisha.