Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya mawasiliano Yas kwa kushirikiana na Samsung, zimezindua rasmi simu janja mpya aina ya Samsung Galaxy A07 na A17, hatua inayolenga kuchochea matumizi ya simu janja na kukuza ujumuishaji wa kidijitali nchini.
Kupitia ushirikiano huo, simu hizo zinapatikana katika maduka yote ya Yas nchini, zikiwa zimeambatana na vifurushi vya kipekee vya data kwa mwaka mzima – GB 78 kwa Galaxy A07 na GB 96 kwa Galaxy A17.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Meneja wa Huduma kwa Vijana na Wateja Maalum Yas, Ikunda Ngowi amesema ushirikiano huo ni uthibitisho wa dhamira ya Yas katika kuwahamasisha Watanzania wengi zaidi kumiliki simu janja ili waweze kunufaika na fursa za kidijitali kupitia huduma bora za intaneti kutoka Yas.

“Ushirikiano wetu na Samsung unaonesha dira ya pamoja ya kuongeza matumizi ya simu janja na kukuza ujumuishaji wa kidijitali nchini.
“Ubora wa simu za Samsung unafahamika duniani kote, hivyo niwaombe Watanzania wachangamkie fursa hii adhimu.
“Mteja anaponunua simu hizi ataunganishwa moja kwa moja na kifurushi cha data cha mwaka mzima kutoka Yas ili aweze kufurahia ulimwengu wa kidijitali papo hapo,” amesema Ngowi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Biashara ya Simu za Mkononi, Samsung Tanzania, Mgope Kiwanga amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kupanua upatikanaji wa teknolojia bora na kuboresha uzoefu wa kidijitali kwa Watanzania.

“Sisi Samsung tunaamini teknolojia inapaswa kuwa karibu na kila mtanzania.
“Ushirikiano huu na Yas unatuwezesha kuwafikia wateja wengi zaidi kupitia simu hizi zenye viwango vya ubora wa hali ya juu, zikiwa na huduma za mawasiliano ya uhakika.
“Hii ni hatua muhimu katika kukuza upatikanaji wa teknolojia na kuwawezesha Watanzania kuishi kwa ufanisi katika dunia hii ya kidigitali,” amesema Kimwaga.
Kupitia mtandao mpana wa maduka ya Yas nchini, wapenzi wa simu za Samsung wanahakikishiwa urahisi wa kupata simu hizi mpya.

Simu hizo aina ya Galaxy A07 na A17 zitauzwa kwa bei ya shilingi 350,000/- na 550,000/- zikiwa na vifurushi vya data vya GB 78 na GB 96 kwa mwaka.
Yas na Samsung zinaendelea kuwa kinara katika kuchochea fursa za kidijitali nchini.
Lakini pia, kusaidia ajenda ya Serikali ya mabadiliko ya kidijitali kwa kupanua upatikanaji wa huduma za intaneti na teknolojia ili kuboresha maisha ya kila Mtanzania.


More Stories
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi
Waziri Mkuu kuanza ziara mkoani Rukwa Marchi 8 Hadi 10