January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yanga yazoa milioni 50/- za Goli la Mama kwenye michezo miwili

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

KLABU ya Yanga imeweza kuzoa kitita cha sh. milioni 50 katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa, dhibi ya Mabingwa wa Burundi Vitalio ambao wamefurushwa kwenye michuano hiyo kwa kipigo cha magoli 10-0.

Huo ni mwendelezo wa utaratibu wa Rais Samhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambapo anatoa sh. milioni 5 kwa kila goli linalofungwa katika hatua ya awali .

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Chamazi, Yanga iliibuka na ushindi wa mabao manne kwa kuichapa Vital’o ambayo ilikuwa mwenyeji kwenye mchezo huo na kukabidhiwa sh. milioni 20 kutoka kwenye Pochi la Mama.

Katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye Uwanja huo huo, Jumamosi jioni timu hiyo ikiwa mwenyeji iliicharaza Vital’o kwa mabao 6-0 na hivyo kuibuka na kitita cha sh. milioni 30.

Akizungumza katika makabidhiano ya fedha hizo mwishoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, alisema Mama hana mbambamba katika kukamilisha ahadi yake kwa timu za Tanzania ambazo ni Yanga, Simba, Azam FC (imetolewa juzi) na Coastal Union ambazo zinawakilisha nchi katika michuano ya kimataifa.

“Mama hana mbambamba, ukifunga lazima upate zawadi yako, kama ilivyokuwa kwa Yanga ambao leo (Jumamosi) wamevuna s.h Milioni 30 kutoka kwa Rais wetu wa nchi.

“Katika mechi ya kwanza Yanga walivuna Milioni 20 kwa magoli yao manne, hivyo ukichanganya na ushindi wao wa bao sita waliopata, timu hii itakuwa imevuna sh milioni 50 kutoka kwa Rais Samia, kama zawadi yao nono ya Goli la Mama,” Alisema Msigwa.

Rais wa Yanga, Eng Hers Said, akionyesha kiasi cha Sh milioni 30 alizokabidhiwa ma Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, kama zawadi ya Goli la Mama, Rais Samia Suluhu Hassan, baada ya timu hiyo kushinda bao 6-0 dhidi ya Vitalo’O FC ya Burundi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Naye Rais wa Yanga, Eng Hers Said, alisema amewataka wachezaji wao wacheze kwa bidii ili wapate magoli mengi, wakiamini watatumia fedha hizo kama sehemu ya bonasi kwa vijana wao.

“Niliwaambia wachezaji wetu nyie chezeni kwa nguvu mpate magoli mengi kwa sababu bonasi anayo Rais Samia, ambapo amekuwa na utaratibu mzuri wa kutoa zawadi kwa timu za Tanzania zinazofanya vizuri, Alisema Said.

Rais huyo wa Yanga mwenye mafanikio makubwa tangu apate nafasi ya kuiongoza klabu hiyo, alisema kila tunda linalopatikana kwa timu za Tanzania, limesababishwa na moyo wa Rais Samia katika kuzitupia macho timu katika mashindano mbalimbali.

Je, Wananchi wataibuka na shilingi ngapi kwenye raundi ya kwanza ambapo itacheza dhidi ya CBE ya Ethiopia? Jibu hilo ni suala la muda. Katika mchezo huo wa Yanga dhidi ya CBE, Klabu hiyo ya Jangwani inatarajia kuanzia ugenini.