January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri afanya mazungumzo na wasanii wa tamthiliya ya HUBA

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuinua na kukuza Tasnia ya Filamu ili kutangaza fursa zilizopo hapa nchini ili kuwawezesha Wadau wa Tasnia kufaidika zaidi na kazi zao.

Mchengerwa ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokutana na Waandishi wa Habari alipokuwa akiagana na Wasanii wa Tamthilia ya Huba inayorushwa na kituo cha DSTV waliokuwa wakielekea Jijini Dubai katika Falme za kiarabu (UAE) baada ya kualikwa kwenda kutekeleza majukumu yao ya kikazi.

Alisema wasanii hao wamekuwa wakifanya juhudi kubwa ambazo zimekuwa zikifanyika katika kazi za Tamthilia hiyo na kuwataka kusonga zaidi mbele ili kuweza kuikuza Sanaa ya filamu Nchini.

Mchengerwa alisema kuwa Serikali ina dhamiria kuinua na kuendeleza Tasnia ya Filamu nchini kwa kuwa Filamu zetu ni chachu ya kutangaza lugha ya Kiswahili pamoja na Tamaduni zetu.

Alisema ukuaji wa Sekta ya Filamu nchini umeendelea kuonesha taswira chanya na hasa tukiangalia tulipotoka na hapa tulipo.

“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan tayari imetenga fedha za maendeleo ya Sanaa na Michezo kiasi cha Shillingi Billioni 2.5 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Sanaa na Utamaduni,” alisema Mchengerwa.

Na kuongeza kuwa”Ni wakati sasa Serikali inaenda kuwashika mkono Wasanii wetu ili mfike mbali zaidi kwani kwa kipindi kirefu mmefanya kazi kubwa kwa bidii na jitihada zenu binafsi,”alisisitiza

Kwa upande wake Mtayarishaji na Muongozaji wa Tamthilia hiyo Azizi Ahmed ameishukuru Serikali kwa ushirikiano wa kuendeleza na kuiinua Tasnia ya Filamu na kuahidi kuendelea kuitangaza Tanzania ndani na nje ya Nchi kupitia Tamthilia yao.

Awali Rais wa Shirikisho la Filamu Tanzania Elia Mjata aliwapongeza Watayarishaji wa Tamthilia hiyo, na kutoa rai kwa Wadau wengine kuongeza ubunifu katika utendaji wao ili kutayarisha kazi zenye ubora.