Na Joyce Kasiki,Timesmajira online
WIZARA ya Katiba na Sheria imefanikiwa kusuluhisha mgogoro wa madai kati ya Mkurugenzi wa Kampuni ya Core multgeneral Supply Limited, Tanziru Mkakile, na mkandarasi mdogo , Sehewa Chando, baada ya pande zote kufika katika banda la Wizara hiyo wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara na kufikia makubaliano ya namna ya kulipa deni lililokuwa likizozaniwa.
Akizungumza baada ya usuluhishi huo jana Mkakile amesema mgogoro ulitokana na malipo yaliyochelewa baada ya Sehewa Chando kutekeleza kazi ya ukandarasi mdogo.
Amesema kuwa kati ya fedha walizokubaliana kulipana, kiasi cha shilingi milioni sita kilibaki hakijalipwa kutokana na changamoto za kifedha.
Mkakile amesema baada ya kufika Wizara ya Katiba na Sheria walipata fursa ya kusikilizwa na kufikishwa kwenye maelewano yaliyomwezesha mdai kuelewa hali halisi ya deni hilo.
Amesema wamekubaliana kuwa kiasi kilichobaki kitalipwa kwa awamu nne za shilingi milioni 1.5 kila mwisho wa mwezi hadi deni lote litakapokamilika.
Kwa upande wake, Sehewa Chando amesema aliamua kuomba msaada wa kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ili kupata suluhisho la mgogoro huo kwa njia ya maelewano badala ya kuufikisha mahakamani.
Amesema ameridhishwa na namna wizara ilivyoshughulikia suala hilo kwa kuzipa pande zote nafasi ya kusikilizwa na kufikia makubaliano yaliyowekwa kwenye hati ya maandishi, hatua ambayo imeondoa tofauti zilizokuwepo kati yao.
“Usuluhishi huu unaonesha nafasi ya Wizara ya Katiba na Sheria katika kutoa huduma za usuluhishi na kutusaidia wananchi na wafanyabiashara kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo na hivyo kuimarisha upatikanaji wa haki na kupunguza migogoro kufikishwa mahakamani.
Akizungumza baada ya usuluhishi huo, Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Silvester Zakayo, amesema wizara inaendelea kutoa huduma mbalimbali za kisheria kwa wananchi, ikiwemo ushauri wa kisheria na utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR).
Amesema katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara, wizara imefanikiwa kusuluhisha migogoro mbalimbali, ukiwemo mgogoro kati ya Kampuni ya Core Multgeneral Supply Limited na mkandarasi mdogo, Sehewa Chando, ambao ulikuwa umechukua muda bila kupatiwa ufumbuzi.
Wakili Zakayo amesema baada ya kuwasikiliza kwa makini pande zote mbili, walifanikiwa kufikia makubaliano yaliyomaliza mgogoro huo kwa njia ya maelewano.
Amewataka wananchi na wafanyabiashara kutumia zaidi njia mbadala za utatuzi wa migogoro kabla ya kufungua mashauri mahakamani, akieleza kuwa njia hiyo ni ya haraka, yenye gharama nafuu na inayosaidia kudumisha mahusiano kati ya wahusika hata baada ya mgogoro kumalizika.
Ameongeza kuwa usuluhishi pia hulinda siri za wahusika, hususan kwa wafanyabiashara, kwa kuwa taarifa za migogoro hubaki kati ya pande zinazohusika badala ya kuwekwa wazi mahakamani

More Stories
Wizara yasuluhisha mgogoro wa Kampuni na Mkandarasi
FCC yatoa elimu ulinzi wa biashara
Maabara za TARURA nguzo ubora miradi ya barabara