December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Ulizni yajivunia kulinda mipaka,uhuru na usalama wa nchi miaka 60 ya muungano

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WIZARA ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imesema inajivunia mafanikio makubwa katika awamu zote sita za serikali ikiwemo kulinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uhuru, na usalama wa nchi kwani kupitia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),
imechangia katika kujenga uchumi imara ambapo wananchi hujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali bila hofu.

Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Aprili 3,2024 na Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Stergomena Tax wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya muungano.

Dkt.Tax amesema Serikali kupitia Wizara imeendelea kutekeleza, na kuliimarisha Jeshi kwa kulipatia zana na vifaa bora na vya kisasa, rasilimali watu, na nyenzo za kufanyia mazoezi ili kuwa imara wakati wote.

“Ili kuliimarisha Jeshi, Serikali kupitia Wizara imeendelea kuboresha maslahi kwa Wanajeshi na Watumishi wa Umma kadri uwezo wa kifedha unavyoruhusu, kwa kuwapatia makazi bora kwa kuwajengea nyumba, pamoja na stahili mbalimbali, kupandisha vyeo kulingana na sifa, vigezo na taratibu,”amesema.

Amesema kuwa mchango mwingine mkubwa wa Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania katika miaka 60 ya Muungano, ni ulinzi madhubuti wa mipaka yetu, uhuru, na katiba kwani nchi imeendelea kuwa imara na yenye amani katika awamu zote.

Ameeleza mafanikio mengine kuwa ni ushiriki wa Wizara kupitia Taasisi zake, hususan JWTZ katika kukabiliana na majanga au maafa mbalimbali pale yanapotokea.

“Katika kutekeleza jukumu hilo, JWTZ imeendelea kushiriki kikamilifu katika kutoa misaada ya uokoaji na ile ya kibinadamu kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa,”amesema Dkt.Tax.

Dkt.Tax ametaja mafanikio mengine ya wizara hiyo katika miaka 60 ya muungano ni kutungwa kwa Sheria ya JKT Na. 16 ya mwaka 1964 (The National Service Act No. 16 of 1964) ambayo iliwezesha kuanzishwa kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Ambapo Sheria hiyo imefanyiwa marekebisho mbalimbali hadi mabadiliko ya mwaka 2002 na imewezesha kuandikishwa vijana wa kujitolea, na kwa mujibu wa sheria.

Vilevile amesema JKT kupitia SUMAJKT imekuwa ikichangia katika pato la taifa kupitia uzalishaji mali na kulipa kodi stahiki kupitia kampuni zake tanzu na miradi mbalimbali.

Ambapo amesema Shirika limefanikiwa pia kuongeza ajira zilizo rasmi na zisizo rasmi takribani 36,479 (29,758 ajira rasmi, na 6720 ajira zisizo rasmi) kwa vijana wa kitanzania kupitia kampuni zake tanzu, viwanda, na miradi mbalimbali.

“Katika miaka 60 ya Muungano, Wizara ya Ulinzi na JKT kupitia taasisi zake imeendelea kufanya na kuendeleza tafiti na uhawilishaji wa teknolojia kwa ajili ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa matumizi ya kijeshi na kiraia.

Vilevile amesema Serikali kupitia wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, imeendelea kushirikiana na taasisi za kimataifa na kikanda, na nchi rafiki kutekeleza diplomasia ya ulinzi.

“Tunapoadhimisha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, serikali kupitia wizara ya Ulinzi na JKT, imeendeleza pia kudumisha uhusiano na mataifa mbalimbali duniani, kupitia mafunzo na mazoezi ya kijeshi, misaada ya kitaalam, vifaa, zana na mitambo, ubadilishanaji wa wataalam, ubadilishanaji taarifa za uhalifu unaovuka mipaka, shughuli za ulinzi wa amani, mapambano dhidi ya ugaidi, uharamia baharini, uvuvi haramu, na usafirishaji haramu wa binadamu, ushirikiano huu, umesaidia kujenga mahusiano mazuri na nchi husika na kuongeza wigo wa mahusiano ya kijeshi na kutekeleza kwa vitendo makubaliano mbalimbali ya ulinzi wa amani,”amesema Dkt.Tax.

Hata hivyo amesema Kimataifa na kikanda, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia JWTZ inashiriki katika operesheni mbalimbali za Umoja wa mataifa kwa kutoa vikosi vya kulinda Amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Afrika ya Kati, Sudan Kusini, na Lebanon.