November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Nishati, Mtibwa wajadili ujenzi njia ya umeme

📌 Ni ya msongo wa kilovoti 132

📌 Ni kufuatia ombi la Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Mtibwa

📌 Bilioni 28 kutekeleza miradi ya umeme Vijijini Mvomero

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Morogoro

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema, Wizara ya Nishati na Kiwanda cha sukari cha Mtibwa wapo kwenye majadiliano ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 132 ili kukidhi mahitaji ya Kiwanda cha Mtibwa.

Mhe. Bashe ameyasema hayo leo Agosti 03, 2024 katika ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kiwanda cha Mtibwa alipokuwa akizindua bwawa la kumwagilia miwa.

“Tumefanya kikao kidogo na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga kuangalia namna gani umeme mkubwa utafika hapa Mtibwa”, na baada ya majadiliano ya kina utekelezaji utaanza’’’ Amesema Mhe. Bashe.

Ameongeza kuwa majadiliano hayo ya awali yatafungua majadiliano mengine yatakayowezesha umeme waliouomba kiwanda cha Mtibwa kuhakikisha unafika ili kuongeza ufanisi.

Aidha, katika majadiliano ya awali wamekubaliana kutakuwa na makubaliano ya Kiwanda cha Mtibwa kujenga njia hiyo ya umeme kutoka katika kituo cha kupokea na kupoza umeme.

Awali Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mtibwa Sugar Bw.Seif Ally Seif amesema,mradi wa bwawa una pampu sita kati ya hizo zinazofanya kazi ni pampu mbili kutokana na kutokuwepo kwa umeme wa kutosha,

Aliongeza kuwa njia ya umeme iliyokuwepo ni ya msongo wa kilovoti 33 huku mahitaji yakiwa njia ya umeme ya msongo 132 hivyo kuweza kwa pampu zote sita kufanya kazi.

Kwa upande wake Mbunge wa Mvomero, Mhe. Jonas Van Zeeland ameishukuru Serikali kwa kuipatia Wilaya ya Kilombero takribani shilingi Bilioni 28 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya umeme Vijijini wilayani humo.

Ameongeza kuwa kati ya Vijiji 60 ambavyo havikuwa na umeme tayari Vijiji 48 vimeshawashwa umeme.