Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania umefanyika uboreshaji mkubwa wa Ofisi na Makazi ya askari wa Vyombo vya Usalama vya Muungano ambapo kwa sasa Wizara imebadilisha mfumo wa ujenzi wa nyumba za askari wa vyeo mbalimbali kutoka kuwa nyumba za mabati na kuwa nyumba za kisasa.
Hayo yameelezwa jijini hapa leo,Aprili 15,2024 na Waziri wa Wizara hiyo,Mhandisi Hamad Masauni wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano ambapo amesema hadi sasa Jeshi la Polisi limejenga nyumba 10,450 kwa ajili ya makazi ya askari wake.
Pia zimejengwa Zahanati za Jeshi la Polisi 35 katika Mikoa mbalimbali nchini ambazo huduma za matibabu kwa askari wa Jeshi la Polisi, familia zao na raia wa kawaida.
Aidha amezungumzia upande wa uhamiaji ambapo amesema Serikali imeiwezesha kujenga nyumba 454 kwa ajili ya makazi ya Maafisa, Askari na watumishi wake katika Mikoa mbalimbali nchini, ukilinganisha na majengo machache ya Makazi yaliyokuwepo kabla ya Muungano mwaka 1964.
“Ujenzi wa makazi ya Askari umesaidia kuwaweka sehemu moja na kuwa rahisi kupatikana kwa haraka pale wanapohitajika kwa dharura pia, umesaidia kupunguza gharama kwa askari ya kupanga uraiani na kuongeza usalama zaidi kwa askari.
“Aidha, uwepo wa makazi hayo umepunguza malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa askari wanapoishi katika nyumba za uraiani huwafanya kushindwa kutimiza majukumu yao ipasavyo kwa kuhofia usalama wao na familia zao,”amesema Mha.Masauni.
Vilevile amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania, Jeshi la Polisi limefanikiwa kujenga Vituo vya Polisi 485 vya daraja ‘A’, ‘B’ na ‘C’ pamoja na ofisi 20 za Makamanda wa Polisi katika Mikoa mbalimbali nchini.
“Idara ya Uhamiaji imefanikiwa kujenga majengo yake ya Ofisi 65 na kuwa na Ofisi katika Mikoa 31, Wilaya 134 na Vituo 64 vya kuingia na kutoka nchini kwa upande wa Bara na Visiwani, ukilinganisha na vichache vilivyokuwepo kabla ya Muungano,”amesema.
Ameeleza kuwa Ujenzi wa Vituo vya Polisi umesaidia kusogeza huduma za polisi kwa wananchi na kuwafanya wananchi kupata fursa ya kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwani zamani huduma hizo walikuwa wanazipata kwa kutembea umbali mrefu na kuwafanya kubaki na taarifa za matukio waliyosikia au kuona kutokana na kushindwa kuyafikisha kwenye Kituo cha Polisi kwa kuhofia kutembea umbali mrefu kwenda kutoa taarifa.
Hata hivyo Masauni amesema katika miaka 60 ya Muungano ili kuondokana na mfumo tuliorithi wa kikoloni, Jeshi la Polisi katika Maboresho yake limeanzisha programu ya Polisi Jamii ambayo Programu hiyo ndani yake kuna miradi takribani 25 inayotekelezwa Tanzania nzima ikiwepo Ushirikishwaji wa Jamii, Ulinzi Shirikishi,Polisi Kata,Usalama wetu Kwanza na Dawati la Jinsia na Watoto.
“Miradi hiyo imewafanya wananchi kuwa na imani na Jeshi la Polisi na kuwa karibu na hivyo kuwezesha utendaji wake ikiwemo kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu na kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika mitaa.
“Polisi jamii imelisaidia Jeshi la Polisi kuwa na uwezo zaidi wa kubaini na kuzuia uhalifu na kuweka mazingira rafiki baina ya polisi na wananchi katika kupata taarifa za matukio mbalimbali kwenye jamii na kuongeza ufanisi katika majukumu yao,”amesema.
Pia amesema katika kipindi cha miaka 60 ya Muungano, Jeshi la Polisi limefanikiwa kuanzisha Vyuo vipya vya Polisi vitatu (3), ukilinganisha na vyuo viwili vilivyokuwepo kabla ya Muungano.
“Vyuo hivyo ni Chuo cha Polisi Zanzibar, Chuo cha Polisi Kidatu na Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza. Vyuo hivyo vina mitaala mipya inayolenga kuwajengea uwezo askari wa kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu nchini,”amesema.
Hata hivyo amesema Mamlaka imefanikiwa kuboresha huduma ya usajili na utambuzi kwa kuanzisha huduma ya usajili mtandaoni (online registration) ambapo watu 27,973 wameshajisajili na kati ya hao raia ni 25,845 na wageni wakaazi ni 2,128, hatua iliyopunguza wananchi kwenda kusajili ofisi za NIDA.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba