January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi akijibu swali la Mbunge wa Same Magharibi David Mathayo (CCM).

Wizara ya Maji yajipanga kutatua matatizo sugu ya maji

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Wizara hiyo imejipanga kumaliza matatizo sugu ya maji nchini.

Mhandisi Mahundi ametoa kauli hiyo Bungeni jana ,jijini hapa wakati akijbu swali la nyongeza la Mbunge wa Same Magharibi David Mathayo (CCM).

Katika swali hilo Mathayo alitaka kujua namna wizara hiyo ilivyojipanga kutatua tatizo la maji mapema hasa katika mji wa Same.

katika swali la msingi Mbunge huyo ametaka kujua kitu kinachochelewesha mradi mkubwa wa maji wa Same-Mwanga-Korogwe na ni lini utakamilika.

akijibu maswali hayo Naibu Waziri huyo amesema mradi huo ulitarajiwa kukamilika Machi mwaka huu.

Hata hivyo amesema kutokana na kasi ya utekelezaji kutokuwa ya kuridhisha Serikali imesitisha mikataba na wakandarasi Desemba mwaka jana.

Amesema mradi huo wenye kugharamia kiasi cha  shilingi bilioni  262 unahusisha ujenzi wa miundombinu ya chanzo cha maji ,ulazaji wa bomba kilomita 71,vituo vya kusukuma maji vitatu na matanki saba  yenye ujazo kuanzia lita 300,000 hadi milioni tisa na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji kilomita 204.

Amesema wizara hiyo inafanya juhudi kuhakikisha taratibu za kuwapata wakandarasi wapya wa kumalizia kazi za mfumo ya umeme na ulazaji bomba kuu kilomita 34.

“Tunatarajia mradi huu ukamilike mwezi Desemba mwaka huu na utanufaisha wananchi wapatao 438,820 wa mji wa Same-Mwanga na vijiji 38 vya wilaya ya Same,Mwanga na Korogwe.”amesema Mhandisi huyo