January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wizara ya Elimu yatoa maagizo COSTECH

Na Grace Gurisha, TimesMajira OnlineĀ 

WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeshatoa maagizo ya kufanya mapitio ya sheria na sera ya Tume ya Taifa Sayansi na Teknolojia (COSTECH) ili kuhakikisha kwamba inaendana na bunifu zinazoendelea hivi sasa.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri,  Juma Kipanga wakati alipotembelea banda la Costech katika maonesho ya 46 ya Sabasaba yanayoendelea mkoani Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo.

Amesema wakati sheria hiyo inaanzishwa kulikuwa hakuna eneo la ubunifu ndani yake ndiyo maana wanataka kufanya mapitio hayo, kwa sababu wanataka bidhaa zinazobuniwa ziweze kutatua changamoto hapa nchini.

“Tumepiga hatua kama tunavyoona tunatengeneza bidhaa mbalimbali kupitia bunifu zetu za ndani , tulichosisitiza ni kuhakikisha bunifu zao zinawafaidisha wao wenyewe, lakini pia zinaweza kutengeneza ajira kwenye jamii,”amesema  Kipanga 

Hata hivyo, Kipanga amesema wameona wabunifu mbalimbali waliyoendelezwa na COSTECH, kabla ya hapo walikuwa na mfuko wao na pia kuna mashindano yanaitwa makisatu.

“Vyombo vyote hivi vimeundwa kuhakikisha kwamba bunifu pamoja na tafiti zinaweza kukuzwa na kuendelezwa ili badae ziwe bidhaa,” amesema Kipanga

Ki panga ametoa rai na wito kwa COSTECH kuendelea kufanya kazi na kushirikiana kwa sababu Taifa hili litajengwa na watanzania wenyewe na lengo la bunifu hizi ni kuhakikisha zinatatua changamoto.

“Tutatumia bunifu zetu za ndani kwa sababu ni rahisi kupata bidhaa inayoweza kutatua changamoto kwa bei rahisi na pia inaweza kutumika kwa urahisi,”amesemaĀ  KipangaĀ 

Naibu Waziri, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Juma Kipanga akipewa maelezo na Mtafiti kutoka Taasisi ya Kilimo Tanzania (Tari), Magreth Lupembe jinsi teknolojia ya kuzalisha nanasi ndani ya chupa wakati alipotembelea banda la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwenye maonesho ya 46 ya sabasaba, Dar es Salaam.Ā