Na Allan Kitwe, Tabora
HALMASHAURI ya manispaa Tabora imetoa onyo kali kwa watendaji, wakusanyaji mapato, wafanyabiashara na wote waliopewa dhamana ya kusimamia mapato ya halmashauri hiyo watakaobainika kuhusika na upotevu wa mapato hayo.
Onyo hilo limetolewa jana na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa hiyo Ramadhan Kapela alipokuwa akizungumza na madiwani, wataalamu na watendaji wa kata zote katika ukumbi wa manispaa.
Amesema kuwa halmashauri hiyo imefikisha asilimia 51 ya makusanyo ya mapato yake kwa mwaka wa fedha 2024/2025 wakati walitakiwa kuwa wamefikia asilimia 58-59 lakini kutokana na baadhi ya watu kutowajibika ipasavyo wako nyuma.
Kapela ameeleza kuwa licha ya soko kuu kufungwa ili kupisha ujenzi wa soko jipya na wafanyabiashara wote kuhamishwa, zoezi la ukusanyaji mapato linapaswa kuimarishwa na kuwapanga vizuri katika maeneo mengine ili waendelee kulipa.
‘Baadhi ya vyanzo vyetu mapato yapo chini sana, usimamizi hauridhishi na kinachokusanywa kinaingia mifukoni mwa watu, hili halikubaliki, pale stendi kuu ya mabasi kuna mapato mengi lakini hayaonekani, hapa kuna upigaji’, ameeleza.
‘Nimepata taarifa, kuna mgambo anakaa pale getini na kukusanya mapato ya abiria na kuyatia mfukoni, huyu naagiza afukuzwe kazi mara moja na wenzake wote ambao anashirikiana nao’, ameelekeza.

Mstahiki Meya amepongeza usimamizi mzuri wa mapato kwenye vibanda vya biashara, magodauni na vibali vya miradi ya magorofa kwani umeweza kuingiza kiasi cha mil 67 ndani ya wiki 2, ila akatoa onyo kwa wanaokaidi kulipa kwa hiari.
Ameonya kuwa zaidi ya miradi mipya 14 ya magorofa katika manispaa hiyo haina vibali vya ujenzi hivyo akamwagiza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Elias Kayandabila kubaini wote wanaokwamisha zoezi hilo na kuwachukulia hatua.

Mkurugenzi Kayandabila ameeleza kuwa ameshaanza kuchukua hatua dhidi ya wote wanaohujumu mapato ya halmashauri na kuongeza kuwa wataendelea kufuatilia na kuchukua hatua kali zaidi ili kukomesha tabia hiyo.
Aidha amedokeza kuwa mwaka huu wamefanikiwa kununua magari mapya 2 aina ya Toyota Prado na Pick-up kwa kutumia mapato ya ndani ili kuboresha utendaji wa halmashauri hiyo.
More Stories
Mpango mahsusi wa Taifa kuhusu Nishati wajadiliwa
Mwenyekiti CCM, Mbunge Rorya wavuruga mafunzo ya makatibu
Serikali ,Washirika wa Maendeleo waweka mkakati utekelezaji Dira ya 2050