November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wenye uhitaji maalum kunufaika na Serikali mtandao

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline

MAMLAKA ya Serikali Mtandao (e-GA), imeahidi kuendelea kubuni na kuboresha mifumo mbalimbali ya TEHAMA, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za Serikali Mtandao kwa watu wenye mahitaji maalum.

Akizungumza katika Maadhimisho ya wiki ya Viziwi duniani 2023, yanayofanyika kitaifa jijini Mbeya, Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji e-GA CPA Salum Mussa, amesema sheria ya Serikali Mtandao Namba 10 ya Mwaka 2019, inatambua na kuthamini kundi la watu wenye uhitaji maalum katika matumizi ya TEHAMA.

“Kifungu cha 28 (1) cha sheria hii, kinazisisitiza taasisi za umma kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum wanapata uelewa wa kutosha na kuwezeshwa kutumia huduma za Serikali Mtandao, hivyo e-GA ipo tayari kushirikiana na makundi hayo katika kuhakikisha hilo linatekelezeka,”ameeleza CPA Salum.

Amesema kuwa, e-GA itaendelea kushirikiana na makundi mbalimbali ili kuwezesha na kuhakikisha, makundi hayo yananufaika na maendeleo ya TEHAMA katika kuzifikia huduma za Serikali kidijitali popote walipo.

Mkurugenzi huyo pia, amelipongeza Shirikisho la Vyama vya Viziwi Tanzania (SHIVWITA), kwa juhudi inazozifanya ili kuhakikisha viziwi wanapata uelewa kuhusu Serikali Mtandao.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Ushauri na Uelekezi e-GA Bi Johan Valentine , ameeleza kwamba Mamlaka imeshatengeza mfumo maalumu kwa ajili watu wenye ulemavu ili kuisaidia Serikali katika utoaji wa huduma za msingi kwa kundi hilo.

Amebainisha kuwa, mfumo huo maalum umeshaanza majaribio mkoani Mara na unatarajiwa kuzinduliwa mwishoni mwa mwaka huu.

” Mfumo huo lengo lake ni kutambua, kusajili na kuratibu masuala yote ya watu wenye uhitaji maalum, ili kuirahisishia Serikali kupata taarifa sahihi na kupanga mipango ya maendeleo kwa kundi hilo”, amefafanua.

Amesema mfumo huo umesanifiwa na e-GA kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu na utawezesha kufikia kundi hilo nchi nzima.

Naye Meneja Mawasiliano e-GA Bi. Subira Kaswaga, ameeleza kwamba, e-GA imeweka jitihadi kubwa katika kuboresha huduma za Serikali kwenda kwa wananchi kidijitali.

“Hakuna kundi litakaloachwa nyuma katika matumizi ya Serikali Mtandao, mifumo inayosanifiwa inalenga kuwafikia wananchi wote wakiwemo Viziwi, lengo ni kuhakikisha kila mwananchi ikiwa ni pamoja na wale wenye uhitaji maalum wanazifikia huduma hizo kwa urahisi zaidi”, ameeleza.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Viziwi mkoa wa Pwani Zalala Selemani, ameishukuru e-GA kwa kuendelea kutoa mafunzo kwa makundi maalum ili yaweze kuzitumia huduma za Serikali Mtandao.