January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri wa Biashara Z’bar azindua mfumo wa taarifa za biashara

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dar

WAZIRI wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Omar Said Shabaan amezindua mfumo wa taarifa za biashara kwa ajili ya kumuwezesha mfanyabiashara kupata taarifa kwa urahisi .

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Zanzibar Omary Said Shaaban (mwenye kaunda suti) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu wa Wizara ya Viwanda bara Exaud Kigahe katika halfa ya uzinduzi wa 
mfumo wa taarifa za biashara kwa ajili ya  kumuwezesha mfanyabiashara kupata taarifa kwa urahisi .

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika katika Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimatafa DITF yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julias Nyerere Jijini Dar es salaam Shaaban amesema mfumo huo utakwenda kuondoa chagamoto kwa wafanyabishara ambazo wamekuwa wakikutana nazo katika biashara zao .

“Upo umuhimu wa Wafanyabiashara kutumia mfumo wa taarifa za biashara kwani utasaidia kuleta tija na kuondoa changamoto zao mbalimbali”amesema Shaaban

Amesema kupitia mfumo biashara zitafanyika katika mazingira rahisi ikiwa ni pamoja na kuondoa ukilitimba na urasimu uliokuwepo awali.

Aidha alitoa wito kwa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara(TANTRADE) kuhakikisha inaweka taarifa wakati ili kumuwezesha mfanyabiashara aweze kufanya biashara kwa urahisi.

Hata hivyo aliwataka wadau kuunga mkono mfumo huo ikiwemo sekta binafsi kushiriki ipasavyo ili kuteta chachu ya maendeleo.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe aliwataka wafanyabiashara kwenda na wakati na wafanye kazi kisasa kwa kutumia njia ya mtandao.

Amesema biashara kwa njia ya mtandao inasaidia kurahisisha muda na hata kupata wateja wengi tofauti na njia iliyozoeleka.

Awali Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade)Balozi Edwin Rutageruka amesema mfumo huo umeshirikisha bodi mbalimbali ikiwemo bodi ya mkonge,kahawa,na korosho ili ziweze kusaidia katika ukusanyaji wa taarifa.

Alisema mfumo huo unaleta tija na ndio maana hivi sasa umepelekwa katika Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (TanTrade )kwa kuwa wao ndio wadau wakubwa wa wafanyabiashara.