Na WAF- DODOMA.
WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amesema kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ili wananchi waendelee kunufaika na huduma hizo nchini hasa katika maeneo ya pembezoni.
Waziri Ummy amebainisha hayo katika tamko la maadhimisho ya wiki ya Famasi kitaifa iliyoanza Juni 10 mpaka Juni 16, yenye kauli mbiu ya “Kuwa na Mustakabali wa pamoja kwa kuimarisha ushirikiano, Kuongeza ubunifu na kuleta mabadiliko katika huduma za dawa”.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya inatambua mchango wa taaluma hii ya Famasi na itaendelea kuhakikisha kuwa, huduma za dawa na vifaa tiba zinazoboreshwa na kupatikana muda wote kwa wananchi hususan wa maeneo ya pembezoni.” Amesema.
Aliendelea kusema kuwa, pamoja na kutambua mchango wa Wafamasia katika utendaji, yapo maeneo yanayohitaji kuboreshwa ili kuhakikisha ubora wa huduma za dawa na vifaa tiba unaendelea kuwa mzuri na wa uhakiki siku zote.
Ili kufikia ubora huo, Waziri Ummy amewataka Wanataaluma kuzingatia uwajibikaji, uadilifu, weledi na kuongeza ubunifu utaosaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za dawa nchini ambazo ni salama, zenye ufanisi na kwa gharama nafuu.
Aidha, Waziri Ummy amesema, bado kuna changamoto ya ukiukaji wa Sheria katika uendeshaji wa huduma za dawa katika maduka ya dawa, kwa kuzingatia athari zinazoambatana na ufunguaji holela wa maduka ya dawa nchini pamoja na uuzaji holela wa dawa kwa wananchi unaosababisha usugu wa vimelea vya maambukizi, gharama za matibabu na wagonjwa kukaa muda mrefu.
Sambamba na hilo amelielekeza Baraza la Famasi na Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) kuendelea kuchukua hatua kwa wote wanaofanya biashara hii kwa udanganyifu bila kufuata Sheria, Miongozo na taratibu zilizowekwa.
“Ninaelekeza vyombo husika hususan Baraza la Famasi na Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) kuendelea kuchukua hatua kwa wale wote wanaofanya biashara kwa udanganyifu bila kufuata utaratibu.” Amesema.
Mbali na hayo ametoa wito kwa wanataaluma wote wa Famasi nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo katika kutoa huduma za dawa, hususan kutouza dawa za cheti (Prescription medicine) kiholela ili kulinda afya za wananchi dhidi ya usugu wa dawa.
Pia, Waziri Ummy amesisitiza kuacha kutumia dawa kiholela bila maelekezo au ushauri kutoka kwa Wataalamu, kwani dawa ni sumu kama itatumika bila kufuata maelekezo.
More Stories
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi
Tanzania yapanda viwango Utawala wa Sheria Duniani
Rais Samia apeleka neema Tabora