Na Mwandishi Wetu,TimesMajira online,Chemba
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu,amesema kuwa hajaridhishwa na usimamizi wa miradi ya afya katika Wilaya ya Chemba Mkoani Dodoma hivyo waliohusika kutafuna fedha katika miradi hiyo atawatafuta popote walipo.
Kauli hiyo ameitoa jana wilayani Chemba Mkoani Dodoma mara baada ya kufanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo Wilayani humo ambapo ametembelea Shule ya Sekondari Chemba ,Hospitali ya Wilaya ya Chemba na Kituo cha Afya cha Hamai.
Waziri Ummy amesema ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Chemba haukusimamiwa vizuri na ndio maana baadhi ya majengo bado hayajakamilika kwa asilimia 100 huku akihoji ni kwanini shilingi milioni 250 zilirudishwa hazina wakati ujenzi haujakamilika.
“Lazima tukubali ujenzi haukusimamiwa vizuri hakukuwa na usimamizi mzuri wanaohusika na manunuzi hawakusimamia vizuri ndio maana milioni 250 zikarudi lakini hapa hakuna hata wagonjwa kwa sababu huduma muhimu hakuna,mna wagonjwa 1000 tu katika Hospitali ya Wilaya kuna shida,”amesema Ummy.
Amesema wote waliohusika na wizi katika miradi hiyo atahakikisha anawawajibisha hata kama wamehama katika Halmashauri hiyo.
“Hii miradi imehujumiwa watu wametanguliza maslahi binafsi najua Mhadhisi aliondolewa ili watu wapige ninayomajina wameharibu wamepelekwa kwingine sasa hata kama ulihamishwa mimi hili siliachi,tukidhibitisha tunakupeleka mahakamani,”amesema.
Hata hivyo Ummy ametoa onyo kwa Watumishi wa TAMISEMI watakaoharibu katika kituo chake cha kazi hataruhusu ahame isipokua atamuwajibisha akiwa katika kituo chake cha kazi.
“Sitaruhusu mtumishi aharibu Chemba kisha ahamishiwe Kongwa, niwahakikishie kuwa ntamshughulikia akiwa hapa hapa Chemba na nikibaini ana hatia ntamchukulia hatua stahiki” amesisitiza Ummy.
Akiwa katika kituo cha afya cha Hamai,Waziri Ummy alipokelewa na wakazi wa vijiji vya Songolo na Hamai ambapo walidai huduma muhimu katika kituo hicho hazipatikani kama Xray,dawa,maji,ambulance,wodi ya wanaume pamoja na uzio.
Katika hatua nyingine Mhe.Ummy amewataka Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kuchapa kazi kama awali na sio kukaa kusubiria uteuzi.
“Hali inayoendelea kwa viongozi hawa haileti afya, wengine hawafanyi kazi eti wanasubiria mkeka, hamuoni kuwa mnaonea wananchi kupata haki yao ya msingi ya kuhudumiwa” alihoji Waziri Ummy.
Kwa upande wake,Mkuu wa Mkoa wa Dodoma,Dk.Binilith Mahenge amesema atahakikisha maji yanapatikana katika Hospitali ya Wilaya na katika kituo cha afya cha Hamai.
More Stories
CCM hakuna kulala, Nchimbi atua Tabora kwa ziara ya siku mbili
Kongamano la Uwekezaji na Biashara lafunguliwa Pwani
Rais Samia afurahia usimamizi mzuri wa miradi