January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ummy: Wanawake wenye macho mekundu hawana mahusiano na imani za kishirikina

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga,

Waziri wa afya Ummy Mwalimu amesema wanawake wenye macho mekundu hawana mahusiano na imani za kishirikina isipokuwa wengine wamepata matatizo ya macho kutokana na matumizi ya kuni.

Pia Waziri Ummy amesema moshi unaotoka kwenye matumizi ya kuni na mikaaa unakwenda kuathiri mifumo ya hewa ikiwemo kupata Saratani ya mfumo wa chakula na hewa, matatizo ya Kifua na macho hivyo ameitaka jamii kutumia nishati ya gesi ili kuondokana na matizo hayo.

Waziri Ummy ametoa kauli hiyo kwenye hafla ya kukabidhi wanawake wajasiriamali mitungi ya gesi na majiko yapatayo 600 kwa wananchi wa jiji la Tanga ikiwa ni mpango wa kupambana na matumizi ya kuni na mkaa unaochangia athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza kwenye hafla Waziri wa Afya na Mbunge wa jimbo la Tanga Ummy Mwalimu amesema hatua hiyo inalenga kukabiliana na wimbi kubwa la matumizi ya nishati ya mkaa na kuni jambo ambalo limekuwa likichangia uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti hovyo.

Waziri Ummy amewataka wanawake kutumia nishati mbadala ya gesi kwenye matumizi ya nyumvani na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo wakati mwingine yanakuwa na gharama kubwa ikilinganishwa na gharama ambayo jamii ingetumia nishati ya gesi.

“Baadhi ya wanawake wanahusishwa na imani za kishirikiana kwa sababu ya kutumia nishati ya kuni hivyo niiase jamii kutumia nishati ya gesi kwani inakwenda kuwasaidia kuondokana na changamoto nyingi, “alisisitiza Waziri Ummy.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya ORYX gas Araman Benoit katika hafla hiyo amesema mpango wa kampuni hiyo ni kutaka kuona kila mtanzania anatumia nishati ya gesi kwa bei nafuu na kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga Hashim Mgandilwa amesema kuwa serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wasambazaji wa gesi ili kuhakikisha wananchi wanaondokana na matumizi ya kuni na hatimaye kutumia nishati ya gesi.

“Kikubwa sisi kama serikali tutaendelea kuwapa ushirikiano ORYX itawasaidia mama zetu adha ya kuugua kifua na mafua kwa matumizi ya kuni na mikaa kwenye majumba yetu hivyo tuwashukuru sana na sisi serikali tutaendelea kuwapa ushirikiano na kuhakikisha ile adhma mliyokuwa nayo mnaweza kuitimiza kwa vitendo, “alisitiza Mgandilwa.

Naye Afisa afya mazingira jiji la Tanga Kizito Mkwabi amesema matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa jambo lililozoeleka kwa jiji la Tanga hasa katika masuala mazima ya mapishi na ujasiriamali mbalimbali unaohusiana na matumizi ya nishati.

“Sisi kama wajasiriamali tuliopo hapa leo hii ni sehemu muhimu sana ikiwezekana kuacha kutumia kuni na mkaa ambazo zimekuwa ni kichocheo kikubwa cha kuharibu nazingira kwa kutumia kuni na mkaa ambazo zinatokana na mazao ya misitu kwani misitu mengi hupotea na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi tunakosa mvua, tunakosa maji, vyanzo vyetu vya maji vinaharibika tunakosa na umeme pia, “alisisitiza Kizito.

Wajasiriamali zaidi ya 600 wa jiji la Tanga wamepatiwa majiko ya gesi yanayotarajiwa kwenda kubadilisha maisha yao.