January 1, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ummy : Magonjwa yasiyo ambukiza bado ni chagamoto katika jamii

Na Mwandishi wetu, Timesmajira online

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amekiri kuwa uwepo wa magonjwa yasiyoambukiza nchini ikiwemo moyo yamekuwa yakimnyima usingizi kutokana na idadi Watanzania kuongezeka.

Waziri Ummy ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo Septemba 29 katika maadhimisho ya siku ya moyo duniani yaliyoambatana na upimaji wananchi katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar Group.

“Suala la moyo au magonjwa yasiyokuambukiza ni jambo ambalo linaninyima usingizi kutokana na ongezeko la Watanzania wenye magonjwa yasiyoambukiza ndio maana nikipata fursa huwa natoa elimu na hamasa kwa Watanzania kuhusu kuchukua hatua mahususi za kujikinga na magonjwa hayo,” amesema

Amesema kwa sasa kuna ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwa shinikizo la juu ya damu ambalo ndilo linasababisha changamoto katika moyo na mishipa ya damu.

Alibainisha kuwa mujibu wa Takwimu za Wizara za Afya zinaonesha kuna ongezeko kubwa la watu wenye magonjwa ya moyo na shinikizo la juu la damu.

Waziri Ummy alifafanua kuwa kwa sasa kumekuwa na ongezeko la asilimia 9.4 kwa wagonjwa ya moyo na shinikizo la damu pekee ambapo mwaka 2017 kulikuwa na wagonjwa milioni 2.5 na mwaka 2022 walikuwewpo milioni 3.4.

Vilevile amesema kuwa Watanzania100 waliofanyiwa uchunguzi, 12 wanao ugonjwa wa kisukari na 25 shinikizo la juu la damu ambalo limebainika kuwa chanzo kikuu cha magonjwa ya moyo, figo na kiharusi.

Aidha aliwataka wananchi wenye matatizo la shinikizo la juu la damu na kisukari kutumia dawa kama walivyoshauriwa na daktari kwani wanapoacha huwasababishia kupata matatizo ya moyo, kiharusi au figo kwa urahisi.

Katika hatua nyingine Waziri Ummy aliiupongeza uongozi wa JKCI kwa kutoa huduma za moyo kwa wananchi kwani uwepo wake umepunguza idadi ya wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi kwa asilimia 80.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Angela Muhozya amesa taasisi ya moyo makao makuu imekuwa ikipokea jumla ya wagonjwa 1500 kwa kila robo ya mwaka na 500 katika hospitali ya Dar Group jijini Dar es Salaam ndio maana wamekuwa wakiielimisha jamii jinsi ya kujikinga na matatizo ya moyo.

Awali Rais wa Chama cha madaktari wa matatizo ya Moyo nchini, Dk. Robert Mvungi amesema tatizo la moyo limekuwa kubwa duniani na tafiti zinaonesha watu milioni 20 duniani wamekuwa wakifa kila mwaka kwa matatizo ya moyo.

Amesema Nchini Tanzania tatizo ni kubwa na utafiti unaonesha asilimia 13 ya Watanzania hufa na ugonjwa ya moyo

Akitaja visababishi vinavyosababisha magonjwa hayo ni pamoja na uzito uliopindukia, shinikizo la damu, kisukari, kutokufanya mazoezi pamoja na uvutaji wa sigara na shisha

“Tafiti zinaonesha kuwa asilimia 80 ya matatizo hayo yanaweza kukigwa kwa fuata ushauri wa daktari pamoja na kupitia afya mara kwa mara.