November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ulega azindua zoezi la uvuvi katika Ziwa Tanganyika

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amezindua zoezi la uvuvi katika  Ziwa Tanganyika baada ya kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi katika ziwa hilo  kwa miezi mitatu.

Waziri Ulega amezindua zoezi hilo katika Mwalo wa Katonga manispaa ya Kihoma Ujiji  mkoani Kigoma Agosti 15 na kubainisha kuwa kupumzishwa kwa shughuli za uvuvi kwa miezi mitatu  kulikuwa kunalenga kulinda rasilimali za uvuvi kwenye ziwa hilo.

Waziri Ulega alisema kuwa kipindi kilichotumika kupumzisha shughuli za uvuvi  kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu samaki wanazaliana kwa wingi na kukua hivyo kuwezesha rasilimali za uvuvi kunufaisha idadi kubwa ya Watanzania.

Amesema uamuzi huo wa kupumzisha ziwa ni utekelezaji wa Mkataba wa Kikanda wa Nchi Wanachama wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) Unaoweka Hatua za Usimamizi wa Uvuvi Endelevu katika Ziwa Tanganyika na Bonde lake. 

 Aidha, Waziri Ulega ametumia  jukwaa hilo kuwaelekeza wavuvi kuwa kufunguliwa kwa shughuli za uvuvi kuendane na matumizi sahihi ya zana na njia halali zinazokubalika kisheria ili samaki walioachwa wazaliane na kukua waendelee kupatikana. 

Waziri huyo wa mifugo na uvuvi alisema kuwa haitakuwa na maana serikali kutumia mitutu ya bunduki kuzuia watu wasivue wakati wa kupumzishwa kwa ziwa wala haina maana ya kuwakomoa watu kwani jambo hilo la kupumzishwa shughuli za uvuvi kunafanywa kwa manufaa ya Watanzania wote na kunafanywa kwa kuwashirikisha wadau wote na wananchi wote.

 Amebainisha kuwa, haitakuwa na maana kama ziwa linapumzishwa kwa ajili ya samaki kuzaliana na kukuwa kwa ustawi wa jamii, halafu linapofunguliwa, samaki waendelee kuvuliwa  kwa njia na zana haramu ambazo zinatishia uendelevu rasilimali hiyo. 

Waziri Ulega amemshukuru  Rais  Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa kipaumbele Sekta ya Uvuvi kwa kuongeza bajeti ya wizara hiyo maradufu  na hivyo kufanya sekta hiyo kuwa na mafanikio yanayoonekana sasa.

Akizungumza katika zoezi hilo Naibu Katibu Mkuu wizara ya mifugo na Uvuvi, Dk.Edwin Mhede alisema kuwa uvuvi imekuwa moja ya sekta kuu ya uchumi nchini ikiajiri watanzania 6000 Sawa na asilimia 10 ya Watanzania wote.

Mhede alisema kuwa katika kipindi cha miaka 10 vyombo vya uvuvi vimeongezeka kwa asilimia saba huku kukiwa na mialo 104 ambayo inahudumia rasilimali za uvuvi katika ziwa Tanganyika.

Mmoja wa wananchi waliohudhuria ufunguzi huo Songoro Athumani anayemiliki mitumbwi ya uvuvi  kutoka kijiji cha Kalilani  wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma alisema wanaunga mkono mpango huo wa serikali wa kupumzisha shughuli za uvuvi kwa muda  kwani umesaidia kuongeza mazao ya uvuvi kutokana na samaki na dagaa kuonekana kwa wingi hata kabla uvuvi haujaanza.