January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Simbachawene: Mashauri ya kesi za ukatili kwa watoto yamalizike ndani ya miezi sita

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mhe. George Simbachawene ameviagiza vyombo vya Sheria kuhakikisha mashauri yote yanayohusu ukatili dhidi ya watoto yanafanyiwa kazi ndani ya miezi 6kwanmuhibu wa Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 huku akitoa onyo kwa wazazi wanaomalizana kifamilia katika mashauri yanayo wahusiana na Ukatili.

Simbachawene ameyaema hayo jana Mei 15, 2022 wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Familia yaliyofanyika jijini Dodoma.

Simbachawene amesema bado kuna familia zinaishi bila amani upendo hali inayosabasha wazazi kutengana na watoto kukosa malezi bora.

Simbachawene amebainisha kuwa hali ya ukatili bado ni mbaya na kwamba matukio mengi hujitokeza kwenye familia ambapo kwa mujibu wa takwimu za kipindi cha Januari hadi Desemba 2021, matukio ya ukatili dhidi ya watoto 11,499 yaliripotiwa.

Ameongeza kuwa kati ya hayo matukio makubwa ni ubakaji 5,899, mimba 1,677 na Ulawiti 1,114 ambapo takwimu hizo zinaonyesha ukatili dhidi ya watoto bado upo licha ya kuwepo makatazo mbalimbali nchini kupitia Serikali na viongozi wa dini.

Simbachawene amesema ili kutatua changamoto hizo kwa sasa Serikali haitomvulia mtu atakayefanya vitendo hivyo kwakuwa vinawanyima haki za msingi za kupata malezi bora.

“Iwe kesi ya ubakaji, ulawiti au mimba naagiza kesi hizo zote iwe kwa DPP, Mahakamani au Polisi mashauri yashughulikiwe ndani ya miezi 6 na wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria, maana ikiachwa hivi yataendelea na hali inatisha kama hatua hazitachukiliwa” alisema Waziri Simbachawene

“Pia natoa onyo kwa familia zenye tabia ya kumalizana kifamilia na wanaofanya hivyo wachukuliwe hatua kwa mujbuwa sheria na mashauri yapelekwe kwenye vyombo vya sheria,”amesisitiza

Simbachawene amewataka watoto wanapofanyiwa vitendo hivyo wasiwe waoga na badala yake watoe taarifa kwa walimu, viongozi wa dini na majirani ili kuokolewa katika changamoto inayoweza kuharibu ndoto zao.

“Watoto msirubuniwe kwa pipi, sh 500 Wala 1000 maana wafanya matukio huwa wanawadanganya kwa viwango hivyo vya fedha na zawadi ndogondogo na ikitokea hali hiyo msiogope kutoa taarifa,”amesisitiza

Awali, akizungumza katika Maadhimisho hayo Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum Dkt. Dorothy Gwajima alisema Wizara hiyo imeandaa mwongozo wa Taifa kuhusu wajibu wa wazazi hususani wanaume kushiriki kwenye malezi ya watoto badala ya kuachia wanawake peke yake.

Ameeleza kuwa Serikali inatambua familia na imekuwa ikiziwezesha kuishi kwa upendo na amani kwa kutoa mafunzo kutoa mafunzo kupitia mataalam wake ambapo wazazi 110,805 wamefikiwa.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Zainab Chaula amesema ili kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya mwaka huu mikoa yote nchini imeagizwa kufanya maadhimisho hayo kwa kuzishirikisha familia kuhusu malezi ya watoto.

Amesema hiyo inatoa fursa kwa wadau kujadili hali ya malezi ya watoto kwa sasa na kuainisha changamoto na kujadili namna ya kuzitatua.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Fatma Mganga amesema familia ni kiini cha kila jambo lakini kuna vibaka, panya road, makahaba na mashoga ambao wanatoka humo huku akieleza kuwa hiyo inasababishwa na mmomonyoko wa maadili.

“Inawezekana Kuna mahali tumetetereka hivyo naomba nitoe rai kwa Wizara husika kwakuwaomba kuhakikisha somo la dini linarudi mashuleni maana haya yanazaliwa kutokana na mmomonyoko wa maadili sababu familia yenye hofu na Mungu haiwezi kufanya mambo kama haya wala kuzalisha watu wa aina hii,”amesema.

Akizungumza wakati wa Kongamano hilo, Mwakilishi Mkazi wa UNICEF, Lawrence Oundo ameshauri kuwa familia ziendelezwe ili ziwe imara kwa kuhakikisha wazazi na walezi wanasaidiwa kwa lengo la kuwa na kizazi chenye malezi Bora na watoto wafikie malengo yao.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia kwa mwaka 2022 yameongozwa na Kaulimbiu “Dumisha Amani na Upendo kwa Familia Imara : Tujitokeze kuhesabiwa”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Gerge Simbachawene, akitoa Hotuba ya Ufunguzi wa Kongamano la Siku ya Familia Duniani, lililo andaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum na kufanyika jijini Dodoma
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima,, akitoa Maelezo ya Utangulizi wakati wa Kongamano kwenye Kongamano la Siku ya Familia lililofanyika jijini Dodoma
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaid Ally Khamis, akitoa Maelezo Mafupi wakati wa Kongamano hilo lililofanyika jijini Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula, akitoa utambulisho na maelezo ya awali kwenye Kongamano hilo lililo andaliwa na Wizara kwa ushirikiano na Wizara za Kisekta ma Mkoa wa Dodoma wakati wa Siku ya Familia
Baadhi ya Wakurugenzi wa Wakuu wa Vitengo kutoka, wakiwa wanafatilia kwa Makini Mijadala ya Kongamano hilo, lililofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma
Baadhi ya Washiriki wa Kongamano hilo wakiwa wanafatilia kwa Makini michango mbali mbali iliyokuwa ikitolewa wakati wa Kongamano hilo.
Mwakilishi wa UNICEF, akitoa ujumbe wake wakati wa Kongamano hilo la Siku ya Familia lililofanyika jijini Dodoma.

Bendi ya Matarumbeta kutoka Kikosi cha Jeshi kikitumbuiza Muda Mfupi kabala yakuanza kwa Kongamano hilo la Siku ya Familia Duniani