December 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaiagiza Bodi ya TTCL kujiendesha kibiashara

Na Penina Malundo, Timesmajira

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari , aliitaka bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania, kwa haraka iwezekanavyo kukaa kutengeneza mpango ambao utawatoa shirika hilo hapo walipo na kuwapeleka katika uendeshaji wa shirika hilo kibiashara.

Maelekezo yake hayo aliyoyatoa kwa mujibu wa sheria kwa Mamlaka ya Kuteua Bodi Chini ya Kifungu cha Tisa cha sheria hiyo ambapo maelekezo hayo yanakuja kutokana na maelekezo mahsusi aliyoyatoa Dkt.Samia Suluhu Hassan Desemba 10,2024,Ikulu ndogo Tungu Zanzibar baada ya kuwaapisha Mawaziri,Manaibu Waziri na Mabalozi wateule.

Waziri Silaa alitoa maagizo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa Uzinduzi wa Bodi hiyo ya TTCL chini ya Mwenyekiti wake mpya,David Nchimbi ambaye aliteuliwa na Rais Samia Septemba 26,mwaka huu.

Silaa amesema maagizo hayo ni ya muda mfupi yanatakiwa kutekelezeka kwa haraka iwezekanavyo ili kuleta mabadiliko katika shirika hilo.

“Naomba myatekeleze haya,niwahaidi milango ya wizara ipo wazi wakati wote tuwasiliane kwa yale ambayo mnadhani majukumu ya bodi yanapaswa kusaidiwa na wizara ili kuweza kutimiza wajibu wetu,ni jukumu langu na watendaji wa wizara kuhakikisha tunalisaidia shirika.

“Uendeshaji wa shirika hili lipo chini ya bodi na Mwenyekiti na wajumbe,leo nimezindua bodi hii na majukumu haya yapo mabegani kwenu matumaini yangu kwa weledi wenu na watu ambao mnauwezo mkubwa na ujuzi mkubwa,”amesema.

Amesema wanatamani kuona,shirika hilo linapaa na kuhakikisha yale ambayo wanatamani kuyaona kwenye shirika yanatimia.”Matumaini yangu kwa jinsi ninavyowafahamu na kuwaona nia yenu tunaweza kufika mbali pale tunapopataka.

“Shirika hili la TTCL ni shirika lililotangulia katika Sekta ya Mawasiliano hivyo Serikali ya Rais Samia imewekeza fedha nyingi sana kwenye miundombinu ya mawasiliano ikiwemo Mkongo wa Taifa ambao kwa sasa umekaribia kuunganisha wilaya zote nchini, pia kuna Miradi mikubwa ikiwemo mradi wa minara ya mawasiliano, Mradi wa International Data centre ambayo ni Data centre ya kisasa kabisaa,”alisema.

Waziri Silaa amesema anaamini kuwa nia ya Rais Samia katika uwekezaji uliofanywa katika miradi hiyo kwa kutumia fedha za umma,unaenda kuleta tija sio tu kwa shirika au kujiendesha kibiashara bali unakuwa na thamani kwenye sekta nyingine.

Amesema shirika hilo likiendeshwa vema linauwezo wa kusaidia sekta ya mawasiliano na tehama katika wizara wezeshi kwani wizara nyingi inategemea wizara hiyo katika kukuza mawasiliano yake na kukuza sekta ya tehama nchini.

“Shirika hili likiendeshwa vema itaweza kusaidia sekta nzima ya uendeshaji serikalini ,sekta ya umma pamoja na sekta nyingine ambazo zinaleta tija katika ukuaji wa uchumi kwa taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL,David Nchimbi amesema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri Silaa na kuyafanyia kazi.” Hakuna ambalo litawashinda ahadi ninayoweza kuitoa ni kwamba tutegemee shirika letu Jipya ,bodi iliyokuwepo mwanzo ilifanya kazi nzuri lakini sisi tutalipeleka shirika mbele zaidi kwa kasi zaidi.

“Tunatambua kiu ya watanzania kuona shirika letub linajiendesha kibiashara na sisi tunachukua changamoto hiyo katika kuchochea maendeleo ya nchi hii kupitia teknolojia ya mawasiliano,”amesema.

Aidha amemshukuru Rais Samia kwa kumteua nafasi hiyo na kumshukuru Waziri Silaa kwa kuteua bodi ya wajumbe hao ambao wanauwezo mkubwa katika utendaji kazi wao.