November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Prof. Mkenda: hatua kali kwa waliovuruga mitihani, wafungwe jela

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali imeweka bayana dhamira ya kuwachukulia hatua kali za uwajibikaji kwa Maafisa Elimu wa Wilaya, Mikoa, Walimu na maafisa wengine wote wakiwemo askari ambao wamepewa jukumu la kusimamia mitihani na badala yake wakafanya udanganyifu.

Akizungumza leo Desemba 5, 2022 jijini Dar es Salaam na uongozi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kampasi ya Mlongazila alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja, Waziri Mkenda amesema hatua kali dhidi ya wasimamizi wa mitihani zitahusisha kusimamishwa kazi, kufukuzwa pamoja na kufikishwa mahakamani ili wafungwe jela.

Aidha, amesema kuwa ili kuimarisha sekta ya elimu lazima kushughulika na watu wanaofanya udanganyifu ikiwemo kuwachukulia hatua kali na kuwajibika huko sio tu kufukuzwa kazi kama ilivyozoeleka au kupewa onyo pekee bali wafungwe jela ili iwe fundisho kwa wengine.

Waziri Mkenda amesema Baraza la Mitihani Tanzania (NACTE) limeongeza mikakati ya kupambana na watu ambao wanafanya udanganyifu kwenye vituo vya mitihani ambapo serikali imewakamata na kuwachukulia hatua wasimamizi wote kwa kushirikiana kufanya ubadhilifu wa mitihani.

Amesema kuwa serikali imechunguza na kubaini kuwa watumishi wa serikali na watumishi wa sekta binafsi wamehusika kwenye udanganyifu wa elimu na kuwachukulia hatua.

“Sasa nisisitize kuna kauli inasema ukitaka kuuwa Taifa basi uwa elimu, sasa tunafanya mageuzi ya elimu nchini kwenye sera na mitaala lakini haiondoi jukumu la kusimamia elimu tunayoitoa sasa hivi inatolewa kwa taratibu zinazokubalika” amesisitiza Mkenda

Hivyo, Waziri Mkenda amesema kuwa udanganyifu katika mitihani una madhara ya kumuwezesha mtu kufaulu ambaye hakustahili kufaulu kwani akiwa daktari ataleta athari kubwa katika jamii.

“Hasara mojawapo kubwa kwa Taifa letu ya kuvujisha mitihani ni kuwafundisha watoto katika umri mdogo kwamba ili uendelee ni lazima ufanye udanganyifu, tunaanza kujenga rushwa mapema mno na serikali haitakubali kitu kama hicho” Amesema Waziri Mkenda