Na Lusungu Helela, WMU
WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Dkt.Damas Ndumbaro amevitaka vyama vingine vya utalii nchini kuiga mfano wa Chama cha Wasafirishaji Watalii (TATO) kwa kuwa ni chama bora cha utalii nchini kwa jinsi kinavyojiendeshwa na kinavyojipanga wakati kinavyowasilisha hoja zake kwa Serikali kwa ajili ya maslahi mapana ya ustawi wa utalii nchini.
Amesema hayo jijini Arusha wakati alipokuwa akizungumza na Bodi ya Wakurugenzi wa Chama cha Wasafrishaji Watalii (TATO) ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kuzungumza na wadau wa utalii nchini.
Amesema, chama hicho ni taasisi imara ambayo ipo kwa ajili ya kuendeleza sekta ya utalii na sio vinginevyo.
Amesema, chama hicho kimekuwa kikijipambanua kwa kuhamasisha wanachama wake kulipa kodi na tozo stahiki za utalii ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali kuhusiana na kukuza na kuendeleza utalii.
Amesema, TATO imekuwa na rekodi nzuri hata pale inapotokea vyama vingine vya utalii vinapogoma kulipa baadhi ya tozo kwa ajili ya utalii na kwenda mahakamani, chama hicho kimekuwa hakiungani navyo kwa ajili ya maslahi ya mapana ya kuendeleza utalii.
Kufuatia rekodi hiyo, Waziri Dkt.Ndumbaro aliwahakikishia Wajumbe wa Bodi wa chama hicho kuwa ataendelea kushirikiana nao na atakuwa akitoa kipaumbele katika kuyashughulikia masuala yao.
“Ninaunda Kamati ya Ushauri ya masula ya Utalii ambayo ninyi kama TATO mtatoa wajumbe watatu na sisi Serikali tunatoa watu watatu kwa ajili kujadili na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazowakabili ikiwemo tozo mbalimbali mnazozilamikia pamoja na suala la masoko,”amesema.
Amesema, kazi ya kamati hiyo itakayoundwa itakuwa ikiishauri Serikali kwa kufanya kazi kwa pamoja na wizara yenye dhamana na utalii kwa lengo la kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini.
“Ninapokuwa na suala nyeti la utalii nimekuwa nikiwashirikisha TATO kutokana na jinsi umakini wao na kujitoa kwao katika suala la utalii,”alilisitiza Dkt.Ndumbaro.
Amesema, licha ya kuwa katika sekta ya utalii kuna vyama vya utalii zaidi ya kumi lakini TATO imekuwa namba moja katika kutafuta suluhu za changamoto badala ya kuwa walalamikaji kama vyama vingine vilivyo.
Amesema, tangu alivyoingia katika wizara hiyo amejionea kuwa chama cha TATO ni chama kilichojijengea heshima na hivyo kuwaahidi kuendeleza ushirikiano na chama hicho.
Katika hatua nyingine, Dkt.Ndumbaro amesema, Wizara ya Maliasili na Utalii imesema ili uweze kuwekeza katika Hifadhi ya Taifa ya Serngeti ni lazima uwe Mwanachama wa TATO ili kuendelea kulinda hadhi na sifa ya hifadhi hiyo duniani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TATO, Willybroad Chamburo alimhakikishia Waziri Dkt.Ndumbaro kuwa, katika uongozi wake wataendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa ajili ya maslahi mapana ya Sekta ya Utalii.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa chama hicho, Chamburo alimshukuru Waziri huyo kwa kukubali kusitisha tozo ya uwekezaji ndani ya Hifadhi za Taifa kwa muda wa miezi mitatu iliyoanza kutumika Julai 1, mwaka huu.
Amesema, kukubali kwake ni ishara tosha ya ushirikiano kati ya chama hicho na Serikali katika kipindi kigumu cha changamoto ya ugonjwa wa UVIKO-19 ulioushambulia sekta ya utalii duniani kote.
More Stories
Mwanasiasa mkongwe afariki Dunia
Rais Samia Kuzindua Sera Mpya ya Elimu na Mafunzo
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM