January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Ndalichako azindua bodi ya Mishahara kwa sekta binafsi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amezindua Bodi ya Mishahara kwa Sekta Binafsi na kuwasisitiza kufanya utafiti na kutoa mapendekezo ya kima cha chini cha mshahara kwa sekta hiyo kitakacho zingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Prof. ndalichako aliyasema hayo wakati akizindua Bodi ya Mishahara kwa Sekta Binafsi katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Osha tarehe 12 April, 2022 jijini Dodoma, ambapo aligusia kima cha chini cha mshahara kuwa ni suala muhimu sana na lazima kuwe na mizani linganifu kwa wafanyakazi ili kuimarisha uchumi shindani wa viwanda kwa maendeleo ya watu.

Aidha alisema bodi hiyo inajukumu la kufanya utafiti, uchunguzi, na kutoa ushauri kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya Kazi kuhusu kima cha chini cha mshahara kisekta.

“Mei Mosi mwaka 2021 Mhe. Rais Samia alizungumzia bodi ya mishahara haijakaa kwa muda mrefu nimeona ni jambo ambalo tulisukume ikiwa ni utekelezaji wa matakwa ya kisheria lakini utekelezaji wa maelekezo ya Rais”. Alisema Prof. Ndalichako.

Alibainisha kuwa muundo wa bodi hiyo una uwakilishi wa utatu ambao ni Serikali, Waajiri na Wafanyakazi ambao wameteuliwa kwa kuzingatia utaalamu wao katika masuala ya Kazi na Ajira.

“Ni matumaini yangu kuwa mtafanikisha utekelezaji kwa kuzingatia kanuni, majadiliano kwa kuwa suala la kufikia kiwango cha mshahara linahitaji majadiliano, pia mzingatie matakwa ya sheria ya kazi na mikataba ya kimataifa ya shirika la Kazi Duniani (ILO)” Alisema Prof. Ndalichako.

Aidha alisema Rais Samia amedhamiria kujenga utumishi wa moyo ili mtumishi aone Fahari kutekeleza majukumu yake pia aliitaka bodi kutoa mapendekezo ambayo yataamsha hali ya kufanya kazi kwa watumishi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vjana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamali Katundu, alisema wajumbe wa bodi hiyo wata andaa Mpango kazi kazi wao kwa kushirikiana na wataalamu ambao utaonesha majukumu watakayo yafanya na lini watatoa mapendekezo ya kima cha chini cha mshahara wa sekta binafsi.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Mohammed Suleiman Rashid aliahidi bodi kufanya kazi kwa umakini na kuzingatia Sheria na taratibu ili lengo linalo kusudiwa lifikiwe.

“ushauri mzuri tutakao utoa utapatikana baada ya sisi wenyewe kufanya utafiti tutateua watu wafanye utafiti na baada ya kuridhika nazo tutakushauri ili utekelezaji wake ulete morali katika Nchi yetu” alisema Prof. Mohammed.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako akiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vjana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamali Katundu (kushoto) katika Mkutano wa Bodi ya Mishahara kwa Sekta Binafsi uliofanyika katika ukumbi wa Osha tarehe 12 April, 2022 jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako akimkabidhi Vitendea Kazi Mwenyekiti wa Bodi kwa Sekta Binafsi Prof. Mohammed Suleiman Rashid katika Mkutano wa Bodi ya Mishahara kwa Sekta Binafsi uliofanyika katika ukumbi wa Osha tarehe 12 April, 2022 jijini Dodoma.
Picha ya pamoja Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako (Katikati) akiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vjana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Jamali Katundu (Kushoto) pamoja na Mwenyekiti wa Bodi kwa Sekta Binafsi Prof. Mohammed Suleiman Rashid (Kulia) pamoja na Kamishna wa kazi Suzan Mkangwa (wa pili kushoto) na wajumbe wa Bodi ya Mishahara kwa Sekta Binafsi.