Na Mbaraka Kambona, TimesMajira Online,Pwani
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan inawajali Wafugaji na ndio maana inaendelea kufanya kila linalowezekana kuwawezesha wafanye shughuli zao kwa tija.
Waziri Ndaki ameyasema hayo juzi katika ziara yake mkoani Morogoro na Pwani ambayo lengo lake lilikuwa kutembelea maeneo yaliyokumbwa na ukame na kuathiri ustawi wa mifugo nchini.
“Rais wetu anawajali wafugaji na ndio maana anafanya kila linalowezekana ikiwemo kuipatia fedha Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili iweze kuwahudumia Wafugaji waweze kufanya shughuli zao kwa tija,” amesema Ndaki.
Amesema katika kuhakikisha Wafugaji wanaendelea kufanya shughuli zao kwa ufanisi, Rais Samia amezielekeza Wizara nane (8) chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuvibakisha katika maeneo yake Vijiji 920 ambavyo vilikuwa na migogoro.
“Rais ameilekeza Wizara ya Ardhi kuweka utaratibu mzuri wa namna ya kuwabakisha wale wanaoishi katika Vijiji hivyo ambapo robo tatu ya maeneo yote ya Vijiji hivyo wanakaa wafugaji,” alifafanua
Aidha, Waziri Ndaki ameongeza kuwa Rais Samia ameridhia kwamba baadhi ya Vijiji ambavyo maeneo yake yalichukuliwa na kufanywa eneo huru la uwindaji yarudishwe kwa wanakijiji ili wayatumie kwa matumizi mengine.
“Nipende kuwahakikishia Wafugaji kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumeanza utaratibu wa kuyarasimisha kisheria kwa kuyatangaza kwenye gazeti la Serikali maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya Wafugaji kwenye Wilaya zenu,” alibainisha.
Pia, Waziri Ndaki amewatahadharisha Wafugaji hao kutoingia kiholela katika vyanzo vya maeneo ya maji, maeneo tengefu kwasababu yanalindwa kisheria na hivyo ni makosa kuingia mifugo yao.
Awali, Mmoja wa Wafugaji kutoka Kijiji cha Kiwege, Kata ya Ngerengere, Mkoani Morogoro, Seif Lekake amemueleza Waziri Ndaki kuwa ukosefu wa miundo mbinu na ufinyu wa maeneo waliyonayo kwa ajili ya kufugia unachangia mifugo kuingia katika maeneo ambayo sio ya ufugaji.
“Waziri tunahitaji msaada wako ili haya maeneo ambayo yametengwa kwa ajili ya Wafugaji yatafutiwe namna ya kupimwa ili yaweze kulindwa kisheria yasiendelee kumegwa kwa sababu baada ya muda yatapotea na Wafugaji wataendelea kutangatanga,” alisema.
Naye, Kaimu Katibu wa Chama cha Wafugaji Wilayani Kibaha, George Mfuko alisema kuwa pamoja na ukame uliyoikumba nchi, matatizo makubwa wanayokumbana nayo Wafugaji ni maeneo ya kufugia na maji ya kunyweshea mifugo na hivyo amemuomba Waziri aweze kuwawekea miundombinu ya maji ili mifugo iwe na uhakika wa maji.
“Katika kipindi hiki cha ukame imefika mahali unanunua dumu la maji la lita mia mbili kwa ajili ya kuwapa mifugo, hili limekuwa ni changamoto kubwa sana kipindi hiki,” amesema.
More Stories
RC Mrindoko:Ufyekaji wa mahindi Tanganyika si maelekezo ya serikali
Walimu S/ Sekondari Ilala wafundwa juu ya maadili ya wanafunzi
Dkt. Samia afungua skuli ya sekondari Misufini, Bumbwini