Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online Mwanza
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, amefurahishwa na hatua iliyofikiwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) katika kupunguza urasimu.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki alipokuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa maonesho ya Biashara, Uwekezaji na Utalii, katika viwanja vya Rock City Mall jijini hapa.
Ameelezea kufurahishwa na hatua hiyo baada ya kupewa ufafanuzi na Ofisa Usajili kutoka BRELA, Gabriel Girangay kuhusu jitihada zilizofanyika kumaliza tatizo hilo alipotembelea Banda la maonesho la BRELA
Girangay amesema BRELA imeboresha huduma inazotoa kwa wadau wake ikiwa ni pamoja na kupunguza muda wa kukamilisha usajili kwa kadri inavyowezekana lakini pia kuwahudumia wateja wote kwa ukaribu kupitia kituo cha miito.
“Kwa sasa muda wa usajili wa jina la biashara ni siku moja na si zaidi ya siku tatu za kazi, usajili wa kampuni ni siku tatu na si zaidi ya siku tano za kazi.
Usajili wa Alama za Biashara na huduma ni kipindi cha siku tisini kutokana na takwa la kisheria,” amesema.
“Maombi ya kupata Hataza ni siku 120 kutokana na takwa la kisheria, kupata leseni ya Kiwanda au Leseni ya Biashara kundi A ni siku moja na si zaidi ya siku tatu za kazi,” alisema.
Akizungumza kenye ufunguzi wa maonesho hayo, Ndaki aliwataka wafanyabiashara na wajasiriamali wa Mkoa wa Mwaza kutumia fursa ya uwepo wa BRELA katika maonesho haya kutatua changamoto zao na kupata elimu.
“Changamoto zinazosemekana zipo katika urasimishaji biashara sasa ndio muda wake kuzimaliza na bahati nzuri BRELA wapo katika maonesho haya, fikeni katika banda lao la maonesho, pateni elimu, wasilisheni changamoto zenu hapo na rasimisheni biashara papo kwa hapo,”amesema Ndaki.
Girangay amesema BRELA inashiriki maonesho haya ikiwa ni sehemu ya mpango wake wa kuwafikia wadau wake katika maeneo yao kwa lengo la kuwapa elimu juu ya umuhimu wa kurasimisha biashara.
Amesema wanaelimisha pia kuhusu, taratibu za urasimishaji biashara na gharama zake, kutatua changamoto na kufanya usajili wa papo kwa hapo.
Maonesho ya Biashara Uwekezaji yaliyoandaliwa na Rock City Mall yanafanyika kwa siku tatu yalianza Aprili 30 na yanatarajiwa kumalizika leo Jumapili.
More Stories
Wakuu wa Wilaya,Wakurugenzi watakiwa kusimamia programu za chakula shuleni
Mbowe akuna wengi kuhusu maridhiano
Waziri Chana amuapisha Kamishna uhifadhi NCAA, ampa maagizo mazito