Na Iddy Lugendo, TimesMajira Online
WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe.Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC) na Wadau wa Tasnia ya Habari katika kuadhimisha Miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambayo yatafanyika Juni 29,2022 SJMC Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo Juni 26,2022 wakati akitoa taarifa hiyo, Amidi, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), Dkt.Mona Mwakalinga amesema lengo la kongamano hilo ni pamoja na kujadili ushiriki wa Shule Kuu nchini katika muktadha wa mashirikiano, changamoto, na fursa za kuweza kufanya kazi pamoja kwa uthabiti zaidi kwa manufaa ya kila upande na Taifa kwa Ujumla.
Amesema Kongamano hilo litakuwa ni wasaa maalum wa kuwakutanisha wahitimu wa Taaluma ya Habari wa TSJ,IJMC na sasa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) yaani Alumni Meet and Greet session, wa miaka mbalimbali kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo kama TSJ na sasa SJMC ya leo.
“Tangu kuanzishwa kwake kama TSJ mwaka 1970, na hadi mwaka 2021 ikiwa SJMC, taasisi hii imeweza kuzalisha wahitimu zaidi ya 3,000 waliomaliza masomo yao katika ngazi ya astashahada,stashahada na shahada za awali, na stashahada na shahada za uzamili”. Amesema Dkt.Mwakalinga.
Aidha washiriki zaidi ya 400 wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo kutoka ndani na nje ya Tanzania hasa wahitimu wa TSJ/IJMC/SJMC, Mawaziri, Wabunge , viongozi na maofisa wa Serikali na wadau wengine wengi wa Habari na Mawasiliano nchini.
More Stories
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha