January 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Nape atoa wito kwa wanahabari, ufunguzi kongamano la SJMC

Na Iddy Lugendo, TimesMajira Online

WAZIRI wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amewataka wanahabari kuweka kipaumbele chao kwa wananchi pindi wanapokuwa wanapeleka Habari jambo ambalo litawajengea heshima katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza katika Konggmano la Kuaadhimisha miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo hicho, iliandaa kongamano hilo Waziri Nape alisema kuwa kipaumbele cha waandishi wa Habari ni wananchi ambao wanapelekewa Habari.

“Kongamano hili limekutanisha wadau muhimu sana katika Tasnia ya Habari ninatamani sana kuona makongamano kama haya yanafanyika ili kujengeana uwezo na kubadilishana mawazo na kipaumbele chetu ni lazima kiwe ni kumfikia mwananchi kwa kumpa Habari sahihi kwa wakati na kumpatia nafasi toshelezi ya kutoa maoni”, Waziri Nape.

Waziri Nape alisema kuwa Bajeti ya Wizara hiyo itatekeleza majukumu ya kuimarisha Tasnia hiyo ili kuiwezesha Tanzania kuimarika kushiriki uchumi wa kidijitali katika kufikia mapinduzi ya nne ya viwanda yanayoendeshwa na Tehama.

Aidha, Waziri Nape amesema kuwa Pamoja na kipaumbele cha Tasnia ya Habari kuwa wananchi ametaja kuwa katika mapinduzi ya uchumi wa kidijitali vyombo vya Habari vinapaswa kuwa sauti ya watu kutoa maoni yao.

Katika kutambua hilo, Waziri Nape alisema Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, inafanya fursa mbalimbali kwa ajili ya kufungua milango ya kuboresha Tasnia hiyo na kuhakikisha kunakuwa na uhuru Zaidi wa Habari na kutoa maoni.

Waziri Nape aliwataka waandaaji wa Kongamano hilo ambalo limefanyika kwa mara ya kwanza katika Maadhimisho ya miaka 60 ya UDSM linakuwa endelevu ili kutoa ujuzi kwa wanahabari chipukizi kutoka kwa wale wakongwe wa Tasnia hiyo.

“Tukiwa na makongamano ya namna hii yatatusaidia kuona mahitaji yaliyoko mtaani na kubadilisha mitaala yetu ili iendenane na kile kilichopo mtaani, ili kile tunachokizalisha kiwe sawa na kilichopo mtaani, naomba kusisitiza kuwa majukumu yetu kama wanahabari ni kupasha Habari kwa weledi na ubora wa hali ya juu kutokana na kile kimefundishwa katika shule za Habari nchini”, amesema Waziri Nape.

Kuhusu Changamoto za Tasnia ya Habari hasa Sheria ya vyombo vya Habari ya 2016, Waziri Nape alisema wadau Pamoja na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari isaidie kutoa maoni yatakayowekwa kwenye sheria hiyo ili kuboresha tasnia na maslahi ya wanahabari kama sheria inavyoeleza.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza katika Kongmano la Kuaadhimisha miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo hicho, iliandaa kongamano hilo ambalo limefanyika leo Juni 29,2022 Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (katikati) akiwa pamoja na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof.William Anangisye (kulia) pamoja na Amidi, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), Dkt.Mona Mwakalinga katika Kongmano la Kuaadhimisha miaka 60 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ambapo Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo hicho, iliandaa kongamano hilo ambalo limefanyika leo Juni 29,2022 Jijini Dar es Salaam