Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima kuwashughulikia watu wanaokwamisha zoezi la urasimishaji anuani za makazi (Post Code) mkoani humo.
Waziri Nape amesema hayo wakati alipotembelea mkoani humo kuangalia maendeleo ya zoezi hilo ambapo Tanga imetajwa kusuasua katika zoezi hilo kulinganisha na mikoa mingine.
“Lengo letu ni pale tulipokwama lazima tutatue, operesheni lazima iwe na wale wanaokwamisha sasa tutaomba watupishe.… Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa, shughulika na wanaojaribu kukwamisha zoezi hili watupishe tuwasaidie.
“Kama wizara tutaongeza nguvu, tutaleta wataalamu kuongeza nguvu kwa sababu hatutaki kushindwa, tunataka wote twende sawa. Hii ni operesheni ya Rais iliyotangazwa na Rais si zoezi la kawaida kwa hiyo msichukulie kawaida. Tunaamini mnaweza, hili ni jambo letu sote,” amesema Nape.
Kwa upande wake RC Malima amekiri kususasua kwa zoezi hilo mkoani Tanga ambapo amezitaja wilaya zilizosababisha hatua hiyo ni Korogwe, Korogwe Mji na Kilindi.
Amesema ameshtushwa na hatua hiyo kwani kama mkoa walikuwa wamejipanga na kila mmoja alipewa majukumu yake ambapo katika hatua nyingine ametoa wiki moja kwa wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watendaji wote wanaosimamia zoezi hilo kuhakikisha hadi ifikapo mwisho wa mwezi huu linakamilika.
“Sasa Mheshimiwa Waziri hili ni la kwangu nalibeba, hatuwezi kupewa maelekezo na Mheshimiwa Rais halafu unakuja huku unakuta jambo kama hili. Nimeshawapa malengo leo nataka hadi kufikia Aprili 18, wiki moja kutoka leo kila mwenye kolamu yake awe amekamilisha na naomba Mheshimiwa Waziri mpelekee salamu zetu Mheshimiwa Rais kuwa hatujamuangusha na hatutamuangusha.
“Na hii operesheni ya anuani na makazi ambayo mimi nimepewa dhamana, nikawaamini wenzangu wakaniangusha, sasa kulingana na maeneo yote naomba nikuhakikishie sasa tupo asilimia 30 tutakwenda zaidi ya asilimia 70 lakini malengo yetu ni kuwa ifikapo mwisho wa mwezi huu tuwe tumekamilisha zoezi hili,” amesema Malima.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Jim Yonazi alisema wizara hiyo imetoa mwongozo nchi nzima ambayo itasaidia katika kutekeleza zoezi hilo ambapo imesambazwa kila mahali katika halmashauri huku akisisitiza fedha za kutekeleza zoezi hilo zipo ili kuhakikisha kazi zinakwenda vizuri.
“Tunalo lengo la kuhakikisha kwamba ifikapo Mei 22 mwaka huu, tunakamilisha zoezi hili na sisi wizara tumejipanga kwenye hilo kwa kushirikiana na wenzetu wa serikali mtandao (e-government). Nataka niwahakikishie wakuu wa mikoa support yetu ipo kubwa na ya uhakika, tunao wataalamu wetu wanapatikana saa 24 kwa hiyo pale unapokuwa na changamot,”; alisema Yonaz.
Akizungumzia mchakato wa zoezi hilo, Mratibu wa Urasimishaji Anuani na Makazi mkoani Tanga, Injinia Amon Kyomo, alisema mikakati ya kamati yake ni kuhakikisha timu zilizoandaliwa kwa ajili ya operesheni hiyo kwa kila halmashauri zinasimamiwa kwa ukaribu lakini pia kunakuwa na ongezeko la asilimia isiyopungua tano sawa na ingizo la anuani za makazi 23,200 kwa siku.
“Kutokana na hali hiyo, mkoa unakusudia zoezi hili kukamilika ndani ya siku 20 kuanzia leo (jana) hivyo kukamilika ifikapo Mei Mosi mwaka huu. Kuhusu mfumo, mawasiliano ya mara kwa mara yamekuwa yakifanyika ngazi za wizara, aidha, tumepokea mtaalamu ambaye ameweka makazi katika mkoa wetu kwa ajili ya zoezi hilo,” alisema.
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi