November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Nalichako: Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kukuza uchumi nchini

Na: Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Dodoma

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan inathamini na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Sekta Binafsi katika ukuaji wa ajira na uchumi nchini.

Ameyasema hayo wakati wa Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 63 wa mwaka wa Chama cha Waajiri uliofanyika Jijini Dodoma tarehe Juni 22, 2022. Amefafanua kuwa Sekta Binafsi ni msingi wa ukuaji wa ajira, na ni injini ya uchumi wa nchi yetu.

Mhe. Ndalichako, amefafanua kuwa sekta binafsi inatoa mchango mkubwa katika uzalishaji wa bidhaa na uwekezaji katika sekta za kimkamakati. Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Waajiri wote hususani wa Sekta Binafsi katika kuibua fursa za maendeleo, kujadili changamoto zao na kuzipatia ufumbuzi kwa haraka.

“Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ina imani kubwa na ATE na Waajiri wote katika kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini” amesema Mhe. Prof. Ndalichako.

Ameongeza kuwa Ofisi hiyo imeendelea kushirikiana na Wadau wa Utatu (Serikali, Wafanyakazi na Waajiri) hususani katika kuboresha mahusiano mahali pa kazi na kulinda Sekta Binafsi kama mdau muhimu wa uchumi nchini.

Ameeleza masuala ambayo serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa utatu ni pamoja na mapitio ya Kanuni za Mafao kwa Wastaafu kwa watumishi wote wa Sekta ya Umma na Binafsi. Pia, inaendelea kupanga kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi kwa kushirikiana na wadau.

Mhe. Ndalichako amesema katika Mwaka wa Fedha 2021/2022 Serikali ilipunguza mchango wa Waajiri katika Sekta Binafsi kwenye Mfuko wa Fidia ya Wafanyakazi kutoka asilimia 1% Hadi asilimia 0.6%. Kuanzia Septemba 2021 Serikali ilipunguza adhabu ya kuchelewesha michango kwa mfuko wa fidia kwa Wafanyakazi kutoka 10% iliyokuwa ikitozwa kwa kila mwezi na kuwa 2.0% kwa mwezi.

Amefafanua kuwa, Waajiri wote waliokuwa wamechelewa kulipa michango yao kwa kipindi cha kuanzia tarehe 01 Oktoba, 2017 hadi tarehe 31 Agosti 2021 walisamehewa riba baada ya kulipa michango yao.”

“katika Bajeti Kuu ya Serikali kwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambayo inaendelea kujadiliwa Bungeni Serikali, imependekeza kufuta tozo mbili za (OSHA) ambazo ni Tozo ya Tshs.10,000/= ya kipimo cha mzio, na Tozo ya Tshs. 25,000/= ya kipimo cha kilele cha Upumuaji zilizokuwa zinatozwa kwa kichwa”.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Bi. Suzanne Ndomba – Doran, amebainisha kuwa chama hicho kitaendelea kushirikiana na serikali katika kudumisha ushirikiano wenye tija katika kuimarisha utatu wenye kujenga uchumi kwa Sekta za uzalishaji nchini.

Mkutano huo, ulihudhuriwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi, Mwenyekiti wa Bodi (ATE), Bi. Jayne Nyimbo Taylor, Rais wa (TUCTA), Bw. Tumaini Nyamhokhia, Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Bw. Colnel Magembe, Mwakilishi wa Mkurugenzi Ofisi ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) nchini Tanzania, Kenya, Rwanda na Uganda, Bw. Jealous Chirove, Kamishina wa Kazi, Bi.Suzan Mkangwa, Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi, Bi. Pendo Berege pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi – Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Dhima ya Mkutano huo ni: ‘Kuboresha Sera za Fedha na za Kodi ili kuongeza tija na kuchochea ukuaji wa Sekta za Kiuchumi.’

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akizungumza wakati wa Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 63 wa mwaka wa Chama cha Waajiri uliofanyika Jijini Dodoma tarehe Juni 22, 2022.
Sehemu ya washiriki wa mkutano huo wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi,Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (hayupo pichani) wakati wa Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 63 wa mwaka wa Chama cha Waajiri uliofanyika Jijini Dodoma
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi akieleza jambo wakati wa Mkutano huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Bi. Suzanne Ndomba – Doran akieleza jambo wakati wa Ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 63 wa mwaka wa Chama cha Waajiri uliofanyika Jijini Dodoma tarehe Juni 22, 2022