December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu atoa maagizo kwa wakuu wa mikoa na wilaya

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia matumizi ya vitendea kazi vinavyotolewa na serikali kwa maafisa ugani waliopo katika maeneo yao ili ziweze kuleta tija tarajiwa.

Hayo yamesemwa leo Agosti 8,2024 na Waziri wa nchi ofisi ya Waziri Mkuu kazi vijana ajira na wenye ulemavu,Ridhwan Kikwete ambaye amemwakilisha Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye kilele cha maadhimisho ya maonesho ya wakulima ya nanenene ambayo Kikanda yamefika Jijini Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale.

Kikwete amesema wakuu wa mikoa na wilaya waendelee kusimamia utendaji kazi na kuwawezesha maafisa ugani katika kutekeleza majukumu ya kutoa huduma za ugani kwa wakulima na wafugaji ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao kwenye maeneo yao .

“Hakikisheni maeneo yote yaliyojengwa miundombinu ya umwagiliaji yanatunzwa na kuwekewa utaratibu mzuri ambao utawezesha jamii ya wafugaji na wakulima kuishi kwa amani katika eneo hili ,mwaka juzi Rais alizindua programu ya kuhakikisha jamii hizo wanaishi kwa pamoja na kutegemeana”amesema Kikwete.

Hata hivyo Kikwete ameagiza kwa Tume ya Taifa ya umwagiliaji inapoandaa maandiko yanayohusu maeneo ya wafugaji ihakikishe inazingatia mahitaji ya miundombinu ya kunyweshea mifugo.

Juma Homera ni mkuu wa mkoa wa Mbeya,amesema kuwa maonesho hayo yamekuwa chachu kubwa katika hatua za kimaendeleo kwa mikoa ya nyanda za juu kusini.

Homera amesema kwamba wakulima wasitegemee kilimo cha mvua pekee bali wakeukie kilimo cha umwagiliaji pia katika kujiongezea kipato katika familia zao pia amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza miundombinu ya umwagiliaji na kufanya uzalishaji wa mazao kuzidi kuongozeka.

Naibu waziri wa mifugo na uvuvi,Alexander Mnyeti amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 serikali imetenga fedha kwa ajili ya utafiti katika ziwa Nyasa ili kufuga kwa njia ya vizimba na kusema ufugaji huo Dunia imefikia huko .

“Mwanza ufugaji huu umeleta tija kubwa pamoja na ziwa Tanganyika ufugaju huu wa njia ya vizimba kuleta tija kwa wafugaji na wafanyabiashara na kuhamasisha mikoa ya nyanda za juu kusini kujitokeza kwa wingi kuomba vizimba kwani Mh Rais ametoa vizimba vingi lakini maombi ni machache ukweli maziwa yetu hayana samaki na kuwa bila kuchukua jitihada za makusudi kwa kutumia Teknolojia ya sasa kufuga kisasa huenda maziwa yakabaki ya kupigia picha”amesema Mnyeti.