Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameitaka Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) kulipa uzito wa kutosha suala la Malezi katika mafunzo wanayotoa.
Waziri Mkenda amesema hayo Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani alipotembelea Taasisi hiyo kuangalia utekelezaji wa majukumu yake ambapo amesema walimu wana nafasi kubwa katika malezi ya watoto kwa kuwa watoto wanatumia muda mrefu wakiwa shule hivyo mafunzo ya malezi yakitolewa yatasaidia sana wawapo katika mazingira ya kazi.
“Katika suala la Uongozi na Usimamizi wa Shule, ADEM iangalie namna ya kufundisha masuala ya malezi kwa walimu ili itusaidie kujua tunafanyaje kuwa na taratibu ambazo zitawasaidia walimu kwenye masuala ya malezi. Viongozi wa dini wanafanya hivyo lakini walimu wana nafasi kubwa zaidi,” amesema Mkenda.
Amesema Taifa lolote ili liendelee ni lazima liheshimu elimu na katika kuheshimu elimu ni lazima kuheshimu mwalimu hivyo inasikitisha kuona baadhi ya walimu ambao wanawafanyia ukatili watoto na kushusha hadhi ya mwalimu akitolea mfano tukio la hivi karibuni la mwalimu kumfanyia ukatili mwanafunzi kwa kumchapa viboko kupitiliza.
Aidha Waziri Mkenda amesema wakati Serikali ikiendelea kuleta fedha kwa ajili ya kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji, tujenge mkakati wa kutumia wahitimu katika kuboresha shule zetu kwa kuwa mahitaji yanaongezeka, pia ADEM iwafundishe Walimu na Viongozi wa elimu juu ya utafutaji wa rasilimali ikiwemo ushirikishwaji wa jamii ili kuendelea kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu nchini.
“Tumesema hakuna michango ya lazima lakini tunahimiza michango ya hiyari. Baada ya kuwa Mbunge kampeni yangu ya kwanza ilikuwa kujenga vyoo bora shuleni na nikaandika barua nyumba zote za ibaada kwamba mwisho wa mwaka watu wanapokuja watembelee shule walizosoma kuona kama kuna kitu wanaweza kusaidia na imekua na matokeo chanya,” ameongeza Prof. Mkenda.
Waziri Mkenda ameongeza kuwa Menejimenti ya mitihani ni nzuri na kupongeza Baraza la Mitihani la Taifa, Walimu na Wasimamizi kwa kazi nzuri wanayoifanya.
Pamoja na kazi nzuri inayofanyika Mhe. Mkenda ameilekeza ADEM kufundisha walimu miiko na maadili ya Uongozi ili wachache wanaoshiriki katika udanganyifu wajue kukiuka miiko na maadili ya kiutumishi katika usimamizi wa mitihani kunaweza kusababisha waniafunzi kufaulu kwa udanganyifu.
Naye Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Siston Masanja Mgullah amesema wamekuwa washauri wa nchi jirani katika kuanzisha Taasisi ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu akitolea mfano nchi za Afrika ya Kusini, Angola, Msumbiji, Malawi ambapo matokeo ya ushauri huo yamekuwa mazuri.
Mtendaji mkuu huyo amemshukuru Rais Samia kwa kuwapatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kampasi ya Mbeya na kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jengo la mihadhara Kampasi ya Bagamoyo lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,000.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa