January 15, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mhagama:Wananchi wekezeni katika elimu

Na Mwandishi wetu,Timesmajira

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama, Peramiho amewataka wananchi wa Muhukuru Lilahi kutumia fursa iliyopo kuwapeleka vijana wao  kujiunga katika Chuo cha Maendeleo ya jamii kilichopo katika eneo hilo ili kunufaika  na maarifa na ujuzi mbalimbali unaotolewa.

Waziri ametoa kauli hiyo wakati wa hafla ya uwashaji wa umeme wa (REA) Wakala wa Umeme Vijijini katika kitongoji cha Aboud Jumbe kilichopo Halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini Mkoani Ruvuma ambapo umeme umewashwa katika Chuo hicho cha Maendeleo ya Jamii leo tarehe 16/07/2024.

Umeme utasaidia utoaji wa mafunzo ya ufundi katika chuo hiki kuwa bora na yakisasa zaidi na matokeo yake ni kuandaa vijana wetu kuweza kujiajiri na kuongeza fursa zao za kuweza kuajiriwa.

“Vijana wananafasi ya kutoa mchango mkubwa sana katika ujenzi wa taifa unaohitaji ujuzi wa kisasa unaoendana na mafunzo yatakayotolewa katika chuo hiki ndio maana nasema umeme ni elimu,” amefafanua Waziri Mhagama.

Aidha amewapongeza vijana waliojiunga na Chuo hicho cha Maendeleo ya Jamii kwa kuwa hawajakosea kufanya maamuzi ya kuja kusoma hapa kwa sababu wanaelewa umuhimu  wa elimu.

“Niendelee kuwahamasisha wananchi wa Muhukuru-Lilahi kuitumia fursa hii vyema, Chuo hiki ni uchumi na Chuo hiki ni maendeleo ndio maana kinaitwa Chuo Cha Maendeleo ya Jamii,” amesema Waziri Mhagama.

“Nimemuachia maelekezo Mkuu wa Chuo atengeneze utaratibu na mkakati maalumu kwa vijana wetu kujiunga na chuo hiki nami nitachangia tupate watoto 10 watakaosoma hapa ili wapate elimu ya ujuzi, ameeleza.

Awali Diwani wa Kata ya Muhukuru-Lilahi na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Songea Vijijini Mhe. Simoni Kapinga amesema chuo hicho kinajihusisha na maswala ya kilimo na mifugo hivyo ameomba Serikali kusaidia upatikanaji wa vifaa vya kufundishia vya kisasa ili wananchi nao wahamasike kulima kilimo cha kisasa.

“Kupitia wewe Waziri wa Nchi tunaomba utusaidie tupate gari kwa ajili ya chuo hiki kwa kutusaidia kuzungumza na Waziri Mwenye dhamana,” amesema Kapinga

Awali Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea Mtela Mwapampamba amewaomba wananchi wa Mhukuru-Lilahi kuacha tabia ya kuuza maeneo kiholela kwa sababu wageni wataongezeka, kutokana na mipango ya ujenzi wa kiwanda cha sukari kinachotarajiwa kujengwa katika kijiji jirani.

“Maeneo yetu ya uzalishaji tuliyobaki nayo kwa sasa tuendelee kuyatunza kwa sababu yatatufaa sasa na siku za usoni kutokana na mabadiliko makubwa ya miundo mbinu yanayotarajiwa kutokea .” amesema Katibu Tawala Mwampamba.