Na Mwandishi wetu, Timesmajira
Waziri wa Madini, AnthonyMavunde amesimamisha shughuli za uchimbaji zilizokuwa zikifanywa na kampuni ya G & I Tech Mining Company Ltd kwa kipindi hichi cha masika na pia mpaka pale tathmini ya kitaalam ya mazingira itapokamilika juu ya shughuli za uchimbaji madini kwenye Mto Zila.
Ameyasema hayo Jana tarehe 30 Desemba, 2024 katika kijiji cha Ifumbo, Wilayani Chunya alipotembelea eneo la leseni ya mwekezaji ambalo lilivamiwa na wananchi na kusababisha mgogoro mkubwa na uharibifu wa mali za mwekezaji huyo.
“Tumetembelea maeneo yote mawili, na sote tumejionea hali halisi ya mazingira. Ni dhamira na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Hassan kuona shughuli zote za kiuchumi hususan za madini zinafanyika kwa utulivu bila kuleta migogoro na pasipo kuathiri mazingira ya eneo shughuli zinapofanyika.
Nimesikiliza hoja za wananchi juu ya uharibifu wa mazingira ya Mto Zila,serikali itaunda Timu ya wataalamu kufanya tathmini ya kina ya mazingira juu ya athari zinazoweza kutokea wakati wa uchimbaji wa madini na kwasasa shughuli zote za uchimbaji madini zisimame kipindi hichi cha masika kama NEMC ilivyoelekeza.
Wizara ya Madini kwa kushirikiana na Watalaam wa Mazingira, wataalam wa Mkoa na wananchi katika muda mfupi ujao inakwenda kuunda Timu ya pamoja ya kufanya tathmini ili itueleze kitaalam iwapo shughuli hizi zinaweza kuendelea kufanyika pasipo athari kwenye mazingira ya Mto Zila.
Nitumie fursa hii kuwataka wananchi wote kuacha vitendo vya uvunjifu wa amani na kujichukulia sheria mkononi,tunalaani kitendo cha kuvamia na kuharibu mali za mwekezaji“Amesema Mavunde
Awali, akitoa maelezo ya utangulizi, Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Batenga ameshukuru ujio wa Waziri wa Madini na kusisitiza kwamba sasa anaona mwanga ambao unakwenda kuleta suluhisho la kudumu katika mgogoro baina ya mwekezaji na wananchi wa kijiji cha Ifumbo na kuwa serikali ngazi ya wilaya itaendelea kusimamia sheria na kanuni ili kuhakikisha eneo hilo linakuwa salama muda wote.
Mbunge wa Jimbo la Chunya,Masache Kasaka kwa niaba ya wananchi aliishukuru Serikali kwa namna inavyoshughulikia changamoto za wananchi na kuweka wazi ombi la wananchi ni kuona mazingira ya mto Zila yanatunzwa kwani ni chanzo kikubwa cha maji kwa Wilaya ya Chunya.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amemshukuru Waziri Mavunde kwa kutembelea chunya na kuahidi kwamba atasimamia maelekezo yake ya kuona shughuli za uchimbaji katika mto Zila zinasimama kipindi hichi cha Masika na mpaka pale Watalaam watakapokamilisha taarifa ya tathmini na kutoa mapendekezo.
More Stories
Rais Mwinyi atenga dola Mil. 10 kila mwaka kulipa madeni
RC Mrindoko:Vyombo vya haki jinai shirikianeni kumaliza kesi kwa wakati
RC Katavi ataka huduma ya maji safi na salama iimarishwe kudhibiti Kipindupindu