November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Masauni azindua Bodi ya Taifa ya Parole

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Hamad Masauni amezindua Bodi ya Taifa ya Parole ambao ukisimamiwa na kutekelezwa ipasavyo
utaweza kusaidia kuwarekebisha wafungwa, kupunguza uhalifu nchini na hatimaye kupunguza msongamano magerezani.

Uzinduzi huo ulifanyika Jana Jijini Dar es salaam, katika ukumbi wa mikutano wa idara ya huduma kwa wakimbizi ambapo Waziri Masauni amesema Pamoja na changamoto zilizojitokeza katika uanzishwaji na utekelezaji wa Mpango wa Parole ingawa kwa idadi ndogo ya wafungwa walionufaika na mpango huo, wengi wamekuwa mashahidi na mashuhuda wazuri katika Jamii kwa kuwa na tabia njema na kushiriki vema katika shughuli za ujenzi wa Taifa wakiwa raia wema.

“Ukweli huu unathibitishwa
kwa takwimu zilizopo zinazoonesha kuwa kati ya wafungwa 5,678 walionufaika kwa mpango wa Parole, ni wafungwa 29 tu ambao walikiuka masharti ya Parole”

Tarehe 15 Julai Rais alipokea Taarifa rasmi ya Tume ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai ambayo pamoja na mambo mbalimbali yaliyopendekezwa na
Tume hiyo, suala la kuongezwa wigo wa matumizi ya adhabu mbadala lilizungumziwa.

Kutokana na hivyo, Waziri Masauni amesema Bodi hiyo ya Parole inalo jukumu kubwa la kuhakikisha mapendekezo hayo ya Tume yanatekelezwa kwa weledi mkubwa katika kufanikisha adhma na mwelekeo huu wa Serikali hususani katika eneo la adhabu mbadala ambazo
zikisimamiwa ipasavyo zitasaidia kupunguza msongamo magerezani kwa kiasi kikubwa.

Kadhalika Waziri Masauni amesema Serikali inazitambua changamoto zilizopo katika utekelezaji wa Sheria ya Bodi za
Parole na kwamba zinafanyiwa kazi kwa lengo la kuzitafutia ufumbuzi.

“Changamoto zilizopo katika utekelezaji wa Sheria ya Bodi za Parole ikiwa ni pamoja na ufinyu wa bajeti, vitendea kazi na ufinyu wa wigo wa Sheria ya Bodi za Parole katika kuwawezesha
wafungwa wengi kuhusishwa katika mpango wa Parole.”

Mbali na hayo, Waziri Masauni amewataka wajumbe wa Bodi ya Parole kuishirikisha
jamii kikamilifu katika urekebishaji wa wafungwa hatimaye kupunguza uhalifu na msongomano magerezani.

“Ningependa kusisitiza kuwa
jukumu hili mlilopewa ni la Kitaifa ambapo kila Mtanzania hususani wafungwa walioko magerezani wanategemea kuwa
litasimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi, na hivyo kuishirikisha jamii kikamilifu katika urekebishaji wa wafungwa hatimaye
kupunguza uhalifu na msongomano magerezani.”