November 14, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Makamba kufanya ziara siku 21 katika mikoa 14

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Nishati, January Makamba anatarajia kufanya ziara ya siku 21 kuanzia kesho Julai 11, 2022, katika mikoa 14 na Wilaya 38 kwa lengo la kukagua na kusimamia miradi inayotekelezwa na Wizara hiyo kwa lengo la kuinua uchumi wa Watanzania.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Waziri Makamba amesema kuwa katika ziara yake hiyo atapokea kero na maoni kutoka kwa wananchi ili Serikali iweze kuzitatua

“Nitapita katika maeneo niliyoyataja katika mikoa ya Mara, Mwanza, Geita, Simiyu, Kagera, Shinyanga, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe, Ruvuma, na mwisho ni mkoa wa Mtwara lakini mikoa mingine itahusika katika awamu ijayo, na katika maeneo haya nitazungumza na wananchi na kupokea kero na maoni ili kuimarisha utendaji wa sekta ya nishati nchini”, Alisema Waziri Makamba.

Waziri Makamba alisema Kipaumbele katika ziara hiyo itakuwa ni kuelimisha wananchi kuhusu upatikanaji wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia, usambaaji wa umeme vijijini na Vitongoji pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika katika maeneo tajwa.

Maeneo mengine ya kipaumbele katika ziara hiyo ni uboreshaji wa huduma zinazotolewa na Wizara na Taasisi zake na usambazaji wa mafuta salama na ya bei nafuu kwa wananchi ili kuzuia matumizi ya mafuta machafu ambayo yanasababisha uharibifu wa vyombo vyao vya moyo .

Aidha, Waziri Makamba alisema lengo la jumla la ziara hiyo ni kusogeza huduma za Wizara kwa wananchi hasa wale wa maeneo ya vijijini na pia kuongeza uelewa kwa Watanzania kuhusu sekta ya nishati na mageuzi makubwa yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita Chini ya Uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan yenye lengo la kuhakikisha kwamba sekta ya nishati inachangia katika ukuaji wa uchumi na kuboresha Maisha ya Watanzania