November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Kijaji amshukuru Rais Samia kwa kutoa Bil. 15.42/-

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Dodoma

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi cha sh.  bilioni 15.42 kwa ajili ya ulipaji wa fidia kwa wananchi wa Ludewa kupisha mradi wa Mchuchuma na Liganga.

Amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho za majadiliano na mwekezaji ili kazi ya kuchimba madini hayo ianze.

Dkt.Kijaji ametoa kauli hiyo juzi Bungeni jijini Dodoma  wakati akihitimisha hoja yake ya maombi ya fedha kwa mwaka 2024/2025.

Amesema mbali na kutoa fedha hizo,pia ametoa maelekezo kwamba wananchi hao wanaopewa fidia, wapewe na elimu ili wanapopokea fedha hizo ziweze kubadilisha maisha yao.Mbunge Joseph Kamonga

“Kwa kushirikiana na Mbunge wa Ludewa, Joseph Kamonga,elimu hiyo imefanya kazi ambapo kijiji kimojawapo wameweza kuwekeza kwenye bondi.

Tulikwenda na taasisi zetu za fedha tukatoa elimu na elimu imefanya kazi,

“Naomba niendelee kukushawishi Mbunge endelea na vile vijiji vingine ili maisha yao yaboreke kupitia fedha hizo.”amesisitiza Waziri huyo

Aidha, amesema kazi ya kulipa fidia imemalizika isipokuwa bado  wananchi wachache ambao hawajaonekana ambapo hatua ya pili inayofuata ni kutwaa lile eneo kuwa mali ya Serikali na baada ya hapo nchi itakuwa na bidhaa ya kuipeleka sokoni.

“Bidhaa yetu ni eneo lenye rasimali ya makaa ya mawe pamoja na chuma cha liganga,na serikali kama ambavyo amesema mheshimiwa Rais Dkt.Samia  wiki moja iliyopita ,sasa tunakwenda kuhitimisha majadiliano na mwekezaji wetu huyu ili kazi iendelee,

“Mimi pamoja na Mawaziri wenzangu,Waziri wa Mambo ya Nje anayeshughulika na Diplomasia nje ya mipaka ya Taifa letu tumeendelea kukaa na watu hawa,Waziri wetu wa Madini ,Waziri wa Mipango na Uwekezaji,Waziri wa Fedha  na Mwanasheria Mkuu wa Serikali,

“Tunachokihitaji ni kuhakikisha Taifa letu haliingii kwenye mgogoro mwingine ili tuweze kuanza utekelezaji wa mradi huu,naomba nilihakikishie bunge lako tukufu,hicho ndicho tunachokisimamia ,mradi  huu tunakwenda kuuhitimisha vizuri,Taifa letu libaki salama,mwekezaji kama anawekeza awekeze,kama hawekezi akae pembeni tupate mwekezaji mwingine afanye kazi hii na Taifa letu linufaike na madini haya tuliyonayo.”

Vile vile amesema kwa kuliangalia eneo lote la Liganga na Mchuchuma eneo hilo ni robo tu ambalo lina mkataba na mwekezaji kati ya eneo zima la liganga na mchuchuma.

Amesema eneo linalobaki la asilimia 75 imetengenezwa na kupatikana vitalu 48 ambavyo tayari wapo watanzania wanaofanya utafiti wa kijiolojia na makampuni mawili yamefanikiwa kupata madini ya makaa ya mawe mazuri na yaanza uchimbaji muda mfupi ujao.

“Tunachotaka kukifanya ni kuhakikisha dhamira ya serikali yetu ya kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/2025 juu ya miradi hii ya kielelezo iweze kutekelezwa na athari chanya zipatikane kwa serikali na wananchi kwa ujumla.”amesema Dkt.Kijaji

Dkt.Kijaji amesema miradi hiyo ya kielelezo inaanza utekelezaji,na mradi mwingine ni mradi wa maganga matitu ambapo serikali imeanza kufanya kazi yake,imeshamaliza majadiliano na mwekezaji ndani ya miezi miwili ijayo serikali itasaini mkataba ili aendelee na kazi yake na nchi iendelee kuvuna madini yake .

Awali Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe takwimu za hapa nchini,zaidi ya asilimia 95 ya biashara zote ni ndogo sana lakini mchango wake ni zaidi ya asilimia 35 ya maendeleo hapa nchini ambapo shughuli zake zinafanywa na akina na mama vijana hasa kwenye kilimo.

Amesema Wizara imeanza kupitia sera ya SME ambayo tunataka iendane na mahitaji ya sasa kwenye sekta ya viwanda na biashara.

Pia amesema serikali inajua umuhimu wa usalama na afya ya wananchi pindi bidhaa zinapozalishwa katika viwanda vidogo.

Aidha amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi milioni 300 kwa ajili kuelimisha wafanyabiashara kuandaa bidhaa kwa ubora ambapo Shirila la viwanda vidogo (SIDO) na Shirika la Viwango (TBS)  ili wafanyabiashara waweze kupata nembo ya ubora.