Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) mapema leo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Utalii na Uchumi wa Jamhuri ya Indonesia, Mhe. Sandiaga Salahuddin Uno ambapo wamejadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano katika Sekta ya Maliasili na Utalii.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika jijini Barcelona Hispania, Mhe. Kairuki amesema kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na Indonesia katika masuala ya utangazaji utalii hasa kwa kutumia njia za kidijitali kimataifa, Uhifadhi wa wanyamapori, utoaji huduma kwa wateja na kuvutia mikutano ya kimataifa.
Ametaja maeneo mengine ya ushirikiano kuwa ni mafunzo na kujengeana uwezo akitolea mfano wa mafunzo ya “wellness and spa” na utalii wa matibabu, “Eco tourism,” “Green investment” na kuweka mkazo katika matumizi ya nishati mbadala.
Aidha, ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka nchini Indonesia kuwekeza nchini katika huduma ya malazi kwenye maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji ndani ya hifadhi na nje ya maeneo ya hifadhi.
Kwa upande wake, Waziri wa Utalii na Uchumi wa Jamhuri ya Indonesia, Mhe. Sandiaga Salahuddin Uno amesema kuwa Indonesia inataka kuimarisha mahusiano baina ya nchi ya Indonesia na Tanzania na pia hivi karibuni itakamilisha mchakato wa kusaini Mkataba wa Makubaliano (MOU).
Kikao hicho kimehudhuriwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali Jabir Mwadini, Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi pamoja na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ya Tanzania na Indonesia
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa