January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Kairuki ataka mazao ya misitu kuongeza thamani

Na Martha Fatael, TimesMajira Online, Same

SERIKALI imewataka wadau wa mazao ya misitu kuongeza jitihada katika kuwaelimisha wananchi na wadau wa mazao ya misitu namna ya kuongeza ubunifu na thamani ya mazao hayo kwa kutambua fursa za kibiashara zilizopo.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (Mb) amesema hayo alipotembelea na kukagua mabanda ya Maonyesho yanayoendelea leo Machi 20, katika wiki ya Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji Miti Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika Machi 21 wilayani Same.

Mgeni Rasmi katika Kilele hicho anatarajiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango.

Kairuki anasema uwepo wa Maonyesho hayo unachangia kukua kwa sekta ya misitu nchini ikiwemo wadau na wananchi kupata ufafanuzi mzuri wa mazao yatolewayo na misitu pamoja na viwango vya thamani za mazao hayo.

“Niwapongeze Wizara pamoja na Wadau wa misitu mliojitokeza kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu majukumu yanayotekelezwa na taasisi zenu ikiwemo elimu ya uhifadhi hii inasaidia kupanua Wigo wa uelewa kwa wananchi juu ya nini serikali Yao unafanya” anasema Kaiiruki

Hata hivyo Kairuki amewata wakazi wote wa Wilaya ya Same, Mkoani Kilimanjaro pamoja na Mikoa ya jirani kujitokeza kwa wingi kutembelea mabanda katika maonyesho hayo Ili kutambua fursa zilizopo lakini pia kufahamu kazi kubwa inayofanywa na serikali katika sekta ya misitu

Baadhi ya wakazi wa Same, Hilary Shoo, Mwanaima Juma wameishukuru serikali kwa kupanga Maonyesho na wiki ya misitu kufanyika wilayani humo, kwani wameweza kujifunza ufugaji nyuki na usindikaji wa asali.

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani na Siku ya Upandaji miti Kitaifa hufanyika kila mwaka Machi 21ambapo kwa mwaka huu Tanzania inaadhimisha Kilele hicho kwa kupanda miti pamoja na shughuli nyingine zinazohusiana na misitu.