November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Jafo:Msifanye kazi kwa mazoea

Na Lulu Mussa,TimesMajira online,Dodoma

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amewataka watumishi wa Ofisi yake kufanya kazi kwa uadilifu ili kueleta tija kwa taifa.

Jafo ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais katika mafunzo kuhusu VVU, UKIMWI na Magonjwa sugu yasiyoambukiza mahala pa kazi yaliyofanyika jijini Dodoma jana.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Selemani Jafo akizungumza na watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais katika mafunzo kuhusu VVU, UKIMWI na Magonjwa sugu yasiyoambukiza mahala pa kazi yaliyofanyika jijini Dodoma jana . (PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)

Jafo amewataka watumishi hao kuzingatia uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa shughuli za serikali na kuacha alama ya kudumu yenye ufanisi katika maeneo yao kuleta matokeo chanya.

Ndugu zangu tufanye kazi kwa juhudi na maarifa, kazi zetu ziwe za mfano kila mmoja ajivunie kuacha Legacy katika maeneo ya kazi, tuishi kama familia moja na kuhakikisha tunasukuma mbele gurudumu la Taifa letu” amesisitiza Jafo.

Waziri Jafo amewata watumishi wa Ofisi yake kuacha kufanya kazi kwa mazoea na kuwaagiza kubadilika ili kuleta matokeo chanya katika utekelekezaji wa majukumu yao.

“Sitegemei mkae Ofisini, tokeni mkatatembelee miradi ya maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wetu, fanyeni tathmini na kufuatilia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Ofisi yetu ili iwe na tija” ameongeza Jafo.

Kwa upande Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mary Maganga amewataka watumishi katika Ofisi yake kutimiza wajibu wao, kuishi kama familia moja, kufanya kazi kwa bidii na kuhimiza mazoezi ili kuepukana na magonjwa yanayoambukiza na yale yasioambukizwa.

Watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais wamepatiwa mafunzo kuhusu Magonjwa sugu yasiyoambukiza (MSY) na magonjwa yanayoambukiza (VVU, UKIMWI) kutoka kwa wataalamu wa Lishe kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Madaktari kutoka Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.