Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Selemani Jafo ameiagiza Tume ya Ushindani (FCC) kuhakikisha inafanya ukaguzi kwa wawekezaji wa makampuni yaliyoungana bila kuratibiwa vizuri ili kuona kama wameisababishia Serikali hasara kiasi gani na kufuata taratibu za kisheria.
Dkt. Jafo alitoa agizo hilo alipoitembelea tume hiyo kwa lengo la kujitambulisha na kusalimia watumishi wa tume hiyo, Agosti 12,2024, Jijini Dar es salaam.
Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuondoa wimbi la makampuni yanayoungana kimyakimya bila Serikali kufahamu ambayo yanaisababishia serikali hasara na kuharibu uwekezaji nchini.
Aidha alisema kuwa Tume hiyo ina haja ya kuzitangaza zaidi ili kuweza kupata makampuni ya uwekezaji kutoka nje ya Nchi ili kuweza kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika sekta ya uwekezaji wa viwanda na biashara pamoja na kuunganisha makampuni na kufuatilia muunganiko wao na taarifa zao.
“Namshukuru Rais Samia kwa mikakati aliyoiweka na uwekezaji kufungua uwekezaji amef aya vizuri hivyo sisi wasaidizi wake tuongeze juhudi kuhakikisha mambo yanaenda kwa kasi”
“Nchi yetu mpaka sasa tumepata viwanda 80,000 katika viwanda hivi mama samia livyoingia kulikuwa na viwanda 62000 viwanda vilivyoongezeka katika kipindi cha uongozi wa miaka zaidi ya mitatu ni viwanda 18,000 kati ya viwanda hivyo Rais salivyoingia alikuta viwanda vikubwa 452 sasa viwanda vikubwa vimefika 618 ongezeko la viwanda karibu 166 hii sawa na asilimia 27 ya idadi ya viwanda vyote nchini”
Pia Dkt. Jafo alisema kwa sasa hamu ya uwekezaji imekua kubwa hivyo wanataka kuhakikisha kwamba kila mkoa unapimana kwa kuwa na programu ya miaka 6 kuanzia mwama 2025-2030 ili kila mkoa kwa mwaka angalau uwekeze viwanda angalau vitatu vikubwa, vitano vya kati na 20 vidogo.
“Hamu ya uwekezaji sasa imekua kubwa, tunataka tuhakikishe kila mkoa tupimane ndani tuwe na programu ya miaka 6 kuanzia mwaka 2025 ianze hadi 2030 hivyo kwa kipindi tuangalie nchi yetu jinsi gani kila mkoa inafanya uwekezaji mkubwa katika maeneo mbalimbali, tutakua na programu kwamba kila mkoa kwa mwaka angalau uwekeze viwanda angalau vitatu vikubwa , vitano vya kati na 20 vidogo ambayo itampa karibuni waajiriwa 175,000 kwa mwaka na kwenda kujibu idadi ya wanafunzi 64000 wanaograduate kila mwaka , tunaenda kujibu tatizo la watanzania”
Vilevile Dkt.Jafo alihimiza upendo kwa watumishi wa tume hiyo pamoja na maadili kwani tume hiyo ni tume muhimu na nyeti katika ushindani wa biashara na kwa kuzingatia hayo itaipelekea utendaji kazi wenye ufanisi
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya ushindani (FCC), William Erio alisema alimshukuru Waziri Dk. Jafo kwa ziara hiyo katika ofisi zao, huku akisema wako tayari kushirikiana naye kutimiza azma ya serikali.
Alisema FCC inafanya kazi kubwa ya kuhamasisha ushindani halali nchini, kudhibiti bidhaa bandia, kwa lengo la kulinda soko na kuvutia uwekezaji kwa uwepo mazingira bora ya biashara nchini.
Pia alisema katika kutekeleza hilo wamewezesha maboresho ya sheria kuendana na mazingira ya sasa, hali ambayo imesaidia katika kuwezesha muungano wa kampuni na viwanda, ambavyo vimechochea ukuaji na uwekezaji nchini na kukuza uchumi.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best