January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yapongeza Azania kukopesha wanawake

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameipongeza Benki ya Azania kwa kuongeza fursa ya ukopeshaji Wanawake.

Pongezi hizo amezitoa jijini Dar es salaam Aprili 5, 2023 wakati akizindua akaunti ya ‘Fanikisha Mwanamke Hodari’ yenye lengo la kuwasaidia Wanawake kupata mikopo kwa riba ndogo na kuongeza mitaji yao.

“Kurahisishwa kwa akaunti hii ambayo haihitaji fedha yoyote kufungua na riba yake ni asilimia moja tu bila gharama za makato ya ziada kutawagusa Makundi Maalum mengi hata yule mwenye biashara ya kawaida kabisa” amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Aidha amewahimiza wanaume wenye familia kuwaruhusu wanawake kukopa na kujishughulisha kutafuta kipato ili washirikiane kutunza familia na kuepusha migogoro inayotokana na kuyumba kiuchumi.

Waziri Dkt. Gwajima amesema Serikali itaendelea kuunga mkono jitihada za Wadau wote wanaohakikisha Makundi Maalum yanawezeshwa hasa kiuchumi kwa lengo la kukuza kasi ya Maendeleo na kuimarisha Ustawi ndani ya Jamii.