November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Gekul awataka wanaofanya uvuvi haramu kuacha haraka

Na Mbaraka Kambona,TimesMajira Online,Manyara

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul amewataka wanaojihusisha na uvuvi usiozingatia sheria na taratibu, kuacha mara moja kwani Serikali haitakuwa na huruma kwa watakaokamatwa.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kushoto) akimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Joseph Mkirikiti alipomtembelea ofisini kwake

Gekul ametoa onyo hilo alipokuwa akizungumza na wavuvi wa Mkoa wa Manyara alipofanya ziara mkoani humo juzi.

Kwa mujibu wa Waziri Gekul,katika operesheni ya kupambana na uvuvi haramu iliyopita ilitumika karibu sh.bilioni 1.2 jambo ambalo alisema, halivumiliki na hivyo aliwataka wavuvi kutoa ushirikiano kwa Serikali ili kukomesha vitendo hivyo.

“Hatutavumilia jambo hili liendelee, sisi kama Wizara tumesema ni lazima tupate muarobaini wa uvuvi haramu lakini na nyinyi wavuvi, muwe tayari kutoa ushirikiano kwa serikali ili uvuvi haramu ukomeshwe mara moja,” amesema Gekul.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Pauline Gekul (kulia) akipokea samaki aina sato kutoka kwa Mkurugenzi Idara ya Uvuvi, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magese Bulayi alipotembelea Kampuni ya XIN SI LU kutoka China iliyowekeza katika ufugaji wa samaki kwenye mabwawa mkoani Manyara juzi

Ameongeza kuwa uvuvi haramu ukikomeshwa, itasaidia kuokoa mazalia ya samaki na kuongeza idadi ya samaki katika maziwa na maeneo mengine.

“Kwa kuwa mmeonesha nia ya kutoa ushirikiano katika hili, shirikianeni na viongozi wenu kuanzia sasa, hizo nyavu haramu zikatupwe, tusisikie tena kuhusu nyavu haramu iwe mwanzo na mwisho,” ameongeza.

Waziri Gekul amesema, kipaumbele cha serikali kwa sasa ni kuimarisha ufugaji wa viumbe maji kwa kutumia vizimba na mabwawa jambo ambalo likisimamiwa vizuri, litaongeza ajira kwa wananchi na kupunguza umaskini na kuchochea uchumi wa taifa.

“Niwaombe Wakurugenzi na viongozi wengine wa halmashauri, waangalie uwezekano kwenye zile asilimia kumi zinazotolewa na serikali kwa vijana, wanawake na walemavu badala ya kuwapa mkononi wafanye utafiti ili kujua ujenzi wa mabwawa unagharimu kiasi gani, ili wawajengee mabwawa ya kufugia samaki na tukiweza kufanya hivyo tutakuwa tumepunguza tatizo la ajira,” amesisitiza.

Katika hatua nyingine,Gekul amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri na Maofisa Uvuvi kuwafikia wavuvi wote na kuhakikisha wanalipia leseni za uvuvi, ili kuzuia upotevu wa mapato na kukuza pato la serikali.

“Hili litekelezwe haraka, kila mtu ajisikie vizuri kulipa kodi ya serikali, lipeni kodi na mpatiwe risiti za mashine za elekroniki kwa kufanya hivyo kutazuia upotevu wa mapato ya serikali,” amefafanua.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Babati, Lazaro Twange amesema maelekezo yote yaliyotolewa na Naibu Waziri wameyapokea na watayafanyia kazi kama ilivyoelekezwa, ili sekta ya uvuvi mkoani humo iweze kupiga hatua inayotarajiwa.

“Tutahakikisha wavuvi wote tunawafikia kwa lengo la kutatua kero zinazowakabili, lakini vile vile wale ambao hawana leseni waweze kukata leseni ili serikali iweze kuwatambua na kupata mapato kupitia shughuli za uvuvi,” alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wavuvi Halmashauri ya Babati, Iddi Hassan amesema watafanyiakazi maelekezo na watahakikisha wanashirikiana na serikali ili wavuvi wote wawe na leseni za uvuvi na wataendelea kupambana na uvuvi haramu kwa ajili ya kunusuru viumbe maji na kuendelea kufanya uvuvi endelevu.