November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Dkt. Gwajima: Wanaume unganeni na wanawake kupigania usawa wa kijinsia

Na mwandishi wetu, TimesMajira Online

Wanaume nchini wametakiwa kuungana na wanawake katika kupigania haki za usawa wa kijinsia ili kuweza kuliletea taifa maendeleo kwa kuhakikisha kila mmoja anashiriki kikamilifu kwenye shughuli za uchumi wa Taifa.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifungua semina ya wanawake katika uongozi na siasa nchini Tanzania inayofanyika katika ukumbi wa Hyatt Regency hotel jijini Dar es salaam Juni 08 2022,

Waziri Dkt. Gwajima amesema kwa kipindi kirefu kundi la wanawake limekuwa nyuma kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo mila na desturi ambazo zinarudisha nyuma juhudi za uwepo wa usawa wa Kijinsia.

Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kuwa jitihada za pamoja zinahitajika ili kuweza kuleta usawa wa kijinsia, kwani kama wanawake watakwenda peke yao bado jitihada hizo zinaweza zisifanikiwe, hivyo inahitajika kundi la wanaume watakao kuwa tayari kuungana na wanawake ambao kwa sasa wamekuwa mstari wa mbele kupigania haki hizo.

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa kwa sasa hapa nchini asilimia 51.04, ni kundi la wanawake na asilimia themanini (80%) ya nguvu kazi ya Sekta ya kilimo ambao huzalisha asilimia sitini (60%) ya chakula chote hapa nchini ni wanawake hivyo ili kufikia usawa wa kijinsia lazima wawe bega kwa bega na wanaume.

“Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika mkutano wake na Wanawake uliofanyika tarehe 08 Juni, 2021, Jijini Dodoma, aliahidi kuwa kinara katika kutekeleza eneo namba mbili linalohusu Haki za Kiuchumi kwa Wanawake ili kuhakikisha kuwa Ahadi za Nchi kuhusu eneo hilo zinatekelezwa ifikapo mwaka 2026” amesema Dkt. Gwajima

Dkt. Gwajima amefafanua kuwa, Serikali ya awamu ya sita imeendelea kutambua umuhimu wa Wanawake kupewa fursa kwenye nafasi za Uongozi na Maamuzi na kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uwakilishi.

“Mawaziri wanawake wameongezeka kutoka asilimia 15 kwa mwaka 2005 hadi asilimia 37 kwa mwaka 2022. Wabunge kutoka asilimia 22 hadi kufikia asilimia 36.7 kwa mwaka 2022. Wabunge na Wajumbe wa Baraza la wawakilishi Zanzibar wawakilishi asilimia 38, Mabalozi wanawake kutoka asilimia 3 kwa mwaka 2005 hadi kufikia asilimia 21.4 kwa mwaka 2022, madiwani asilimia 29.9. Aidha, Tanzania imeendelea kuwaamini wanawake na kushuhudia wakiongoza nafasi za juu za kisiasa na utendaji serikalini” alisema Dkt. Gwajima

Awali akitoa salam za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Zena Ahmed Said, alisema katika Siku za hivi karibuni kumekuwepo na jitihada mbali mbali za kuwainua wanawake kwenye nafasi mbali mbali ikiwepo nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi ambayo yeye anayoishikilia kwa sasa ni sehemu ya Historia hiyo lakini nafasi Mkurugenzi wa Mashtaka amabayo nayo inashikiliwa na Mwanamke huko Zanzibar.

Akitoa wasilisho kwenye Semina hiyo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Kadari Singo alisema, zipo jitihada zinazo chukuliwa kuwainua wanawake ambapo kwa sasa kiwango cha wananwake kimeongezeka hadi kufikia asilimia 35 kwenye ngazi za maamuzi.