December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Dkt. Gwajima awataka Jamii kutowaficha watu wanaofanya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amezitaka Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto zinazotekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) kuweka mikakati ya kupambana na vitendo vya ukatili vinavyotokea nchini.

Akifungua kikao na Kamati ya utekelezaji wa MTAKUWWA mkoa wa Dodoma leo tarehe Februari 15, 2022 Mhe. Gwajima amebainisha kuwa moja ya changamoto inayokwamisha utekelezaji wa mpango huo ni kamati za Ulinzi wa Wanawake na watoto katika mitaa na vijiji kutotekeleza majukumu yao.

Waziri Dkt. Gwajima amesema utatuzi wa changamoto za ukatili unahitaji jitihada endelevu za Serikali na jamii yenyewe kwani kama ukatili unafanywa na ndugu wa karibu, jamii inawaficha ili kuwasitiri hivyo kamati zinatakiwa zisimame na kuzungumzia kuhusu ukatili.

“Hofu ya Mungu iwepo ili watu wamrudie Mungu badala ya kuwaogopa binadamu, hatutarajii matukio kutokea na kamati zipo zisiwe na mipango ya kubaini viashiria vya ukatili” alisema Dkt. Gwajima

“Kamati za ulinzi wa wanawake na watoto 18126 zimeanzishwa katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Halmashauri, kata, vijiji na mitaa, mwaka 2021 ikilinganishwa na kamati 16343 mwaka 2019 sawa na ongezeko la Kamati 1843” alisema Dkt. Gwajima

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, Serikali ina wajibu wa kuandaa mikakati madhubuti iliyoboreshwa itakayosiadia kuimarisha Kamati za MTAKUWWA ikiwemo kutenga bajeti kwa kushirikiana na wadau kwa ajili ya utekelezaji wa mpango kazi huo.

Aidha, ameiomba mikoa na Halmashauri nchini kuunda kamati za ulinzi kwa Mwanamke na Mtoto katika ngazi ya Kijiji/Mitaa mahali ambako hazijaundwa kwa kuanza na mkoa wa Dodoma, zipewe majukumu yake kwa usahihi na kufanya kazi kwa tija.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Zainab Chaula amezitaka Kamati kuanzia ngazi ya Taifa kuufanya mpango kazi huu wa Taifa ujioneshe katika matokeo halisi badala ya kubaki kwenye mafaili.

Dkt. Chaula amesema Mpango huo ulianzishwa ikiwa ni msingi wa kutokomeza vitendo vya ukatili na kila sekta inatekeleza hivyo kwa kuanza na Wizara inayosimamia sera na miongozo kuwe na ajenda moja na kila mmoja asimamie eneo alilokasimiwa.

“Kupitia kikao hiki nina imani tutaweka mipango thabiti kuhakikisha vitendo hivi vya ukatili na mauaji vinatokomezwa” alisema Dkt. Chaula

Kwa upande wake Mratibu wa mpango huo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Happiness Mugyabuso amesema katika utekelezaji wa mpango huo ulioanza mwaka 2017/2018 kumekuwa na changamoto nyingi katika jamii japokuwa kumekuwa na mafanikio kutokana na jithada zinazofanywa na Serikali na wadau ikiwemo kuimarisha mifumo ya kitaasisi.

Amesema baadhi ya mifumo hiyo ni pamoja na madawati ya jinsia, vituo vya mkono kwa mkono na nyumba salama kwa lengo la kuwashughulikia waathirika wa matukio ya ukatili.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa Dodoma Bernard Abraham amebainisha kuwa, chanzo kikubwa cha ukatili katika jamii ni uchumi wa kaya kuwa mdogo, hivyo katika utekelezaji wa mpango huu, nguvu kubwa ielekezwe kuimarisha uchumi wa kaya.