January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Dkt. Biteko akabidhi magari 40 kwa Tume ya Madini nchini

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Tume ya Madini imekabidhiwa magari saba kati ya magari 40 yanayotarajiwa kutolewa na Serikali kama moja ya mikakati ya kuboresha mazingira ya ukusanyaji wa maduhuli kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini nchini.

Akizungumza kabla ya kuzindua magari hayo leo tarehe 21 Februari, 2022 Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko mbali na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa magari hayo yatatumika kama kichocheo cha ukusanyaji wa maduhuli kwenye shughuli za uchimbaji na biashara ya madini.

Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kununua vifaa vingine kama vile mashine za kupima madini kwenye masoko ya madini na kusimamia kwa karibu shughuli za madini ili kuhakikisha Serikali inapata mapato yake stahiki.


Aidha, amewataka watendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha magari yanatunzwa na kuendelea kuchapa kazi kwa ubunifu mkubwa ili kuhakikisha lengo la kukusanya shilingi bilioni 650 kwa Mwaka wa fedha 2021/2022 linafikiwa ifikapo mwezi Juni mwaka huu.

Katika hatua nyingine akizungumzia mikakati iliyowekwa na Wizara ya Madini kwenye udhibiti wa utoroshaji wa madini, Dkt. Biteko amesema kuwa mikakati iliyowekwa ni pamoja na kuongeza maafisa kwenye usimamizi wa shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Waziri Biteko amewataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini nchini kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa kufuata sheria na kanuni za madini na kusisitiza kuwa Serikali haitamwonea huruma mtu yeyote ayakayebainika anatorosha madini.

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Tume ya Madini Profesa Idris Kikula sambamba na kuishukuru Wizara ya Madini kwa ununuzi wa magari kwa ajili ya kutumiwa kwenye shughuli za madini amesema kuwa magari yatarahisisha kwa kiasi kikubwa utendaji kazi kwa kufika maeneo yasiyofikika kirahisi.Â