Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amepokea gawio la Serikali la zaidi ya sh. Bilioni 4.35, kutoka Kampuni ya Bomba la Kusafirisha Mafuta la Tanzania – Zambia (TAZAMA) akisema hayo ni matokea ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Zambia .
Dkt. Biteko alipokea gawio jana jijini Dar es Salaam huku akishuhudiwa na viongozi mbalimbali wa nchi hizo mbili ambapo ni miaka mitano tangu kutolewa kwa gawio mwaka 2019.
Alisema mapokezi ya gawio hilo ni matokeo ya ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Zambia ambapo alielekeza miradi isimamiwe vizuri ili ilete matunda na kubadili maisha ya watu wa nchi hizo mbili
“Nawapongeza sana Bodi ya TAZAMA na Wizara ya Nishati kwa hatua hii, haya ni matokeo ya ziara ya Rais nchini Zambia ambapo alituelekeza miradi hii tuisimamie na ilete matunda na kubadili maisha ya watu wa nchi zetu.” Alisema Biteko.
Aidha, aliitaka TAZAMA kuendelea kulisimamia vizuri Bomba hilo ili lizidi kuleta faida ambapo mikakati iliyopo sasa ni kuongeza ukubwa wa bomba la TAZAMA kutoka inchi nane hadi inchi 12.
Pia, alisema kuwa, Serikali za nchi hizo mbili ziko katika hatua za manunuzi kwa ajili ya kujenga bomba kubwa la mafuta lenye kipenyo cha inchi 24, suala litakalopunguza gharama za usafirishaji wa bidhaa hiyo, ikiwa ni pamoja na kulinda miundombinu yake.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo ameeleza kuwa Kampuni hiyo iliyokuwa kwenye hati ya kufa imeonesha kufufuka na kutoa gawio kwa Serikali.
“Tumezoea watu na Mashirika yakiomba pesa kwa Serikali, lakini leo (jana) ni kinyume na tunashuhudia Serikali ikipokea gawio, hilo ni jambo la kujivunia sana.” Amesema Prof. Mkumbo.
Kwa upande wake, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu alisema kwa umri wa Kampuni ya TAZAMA yenye miaka 58 tangu kuanzishwa kwake imeonesha matumaini makubwa kwa kuanza upya kutoa gawio kwa Serikali na hii ni kutokana na utekelezaji wa 4R za Rais Samia Suluhu Hassan.
More Stories
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi
Tanzania yapanda viwango Utawala wa Sheria Duniani
Rais Samia apeleka neema Tabora