November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Bashungwa: Wamachinga wapewe mikopo ya gharama nafuu

Na mwandishi wetu, Timesmajira Online

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Sekta za kifedha na Taasisi binafsi kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kutoa huduma za mikopo ya gharama nafuu kwa ajili ya kukuza biashara za wajasiriamali wadogo.

Akifungua kongamano la Jukwaa la Maendeleo ya Sekta ya Fedha leo tarehe 20 Mei, 2022, Jijini Dodoma Mhe. Bashungwa ameziomba taasisi kuinua kundi hilo kwa lengo kwa kutoa mikopo ili kuboresha mazingira ya biashara na kuinua wigo wa ulipaji kodi.

Bashungwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira ya kutambua Wamachinga kuwa Sekta rasmi na kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya biashara

Amewahakikishia wajasiriamali wadogo (wamachinga) wote nchini kuwa Serikali ina dhamira ya dhati katika kuhakikisha inatengeneza mazingira wezeshi kwa ajili yako kote nchini hivyo Wizara husika zitahakikisha zinatekeleza kwa weledi dhamira ya Rais Samia ya kuleta maisha bora kwa machinga inafanikiwa.

Aidha, amewaagiza Makatibu wa Wizara ya fedha, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsi, wazee na mahitaji Maalum na Ofisi ya Rais TAMISEMI kukaa kwa pamoja ili kujadili na kuchambua maazimio ya kongamano hilo na kupata muelekeo wa Sekta ya Machinga nchini

Bashungwa amesema Sekta ya Machinga ina fursa kubwa katika kuchangia uchumi wa nchi hivyo amewataka viongozi mbalimbali kuhakikisha wanatumia kongamano hilo kujadili kwa kina maeneo yaliyofanywa vizuri katika sekta hiyo, changamaoto zilizopo na fursa za kiuchumi ambazo zikisimamiawa ipasavyo zitaleta mafanikio katika sekta ya Machinga.