December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Bashungwa afanya kikao kazi na Watendaji wote wa Wizara yake.

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Innocent Bashungwa amefanya kikao cha kazi na Menejimenti ya Wizara na Taasisi zake zote kujadili utekelezaji wa kazi leo Novemba 18, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa Wizara hiyo Mtumba mjini Dodoma.

Katika kikao hicho Mhe. Waziri ameambatana na Naibu wake Pauline Gekul, ambaye amemshukuru Mhe. Rais kwa kuendelea kuwaamini kusimamia Wizara hiyo na kuwataka Watendaji kufanya kazi kwa weledi.

Pia, Waziri Bashungwa amewataka Watendaji kuthamini heshima kubwa ambayo Mhe. ameitoa kwa Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kufanya kazi kwa bidii.

Aidha, amemshukuru Katibu Mkuu. Dkt, Hassan Abbasi, kwa ubunifu wake wa kutumia raslimali zilizopo kuleta matokeo makubwa katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Amefafanua kuwa kwa sasa Sekta za Wizara zimekuwa zikionekana na kusikika zikifanya vizuri kuliko awali.

Pamoja na mambo mengine, katika kikao hicho, Waziri amepitishwa kwenye mifumo mipya ya kidigitali ya usimamizi wa taarifa za Msanii (AMIS) Filamu na Hakimiliki iliyotengenezwa na taasisi za Sekta ya Sanaa ambayo itasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Wasanii.

Mifumo hiyo inatarajia kupunguza muda wa utoaji huduma kwa kiasi kikubwa, kuongeza mapato kwa serikali na kusogeza huduma kwa wadau.

Mifumo hii inatarajiwa kuzinduliwa rasmi hivi karibuni ili Wasanii waweze kunufaika na kazi zao na kuboresha maisha yao.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake ya awali aliyoitoa bungeni alifafanua kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inatoa kipaumbele kwa wasanii ili kuongeza ajira kwa vijana na kuboresha maisha yao.

Mambo mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na Taifa CUP na Mashindano ya Mpira wa Miguu kwa Walemavu Afrika (CANAF)